Zao la Parachichi lawekewe utaratibu maalumu wa stakabadhi za ghala

Na. Hamida Ramadhan, RUJAT Dodoma

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeanza mazungumzo na wazalishaji wa parachichi katika wilaya za Mufindi na Njombe kwa lengo la kuanzisha mfumo wa ubunifu utakaoruhusu shamba kutumika kama ghala la bidhaa hai ili kuongeza ufanisi wa biashara ya zao hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amesema hayo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma wakati akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo, aliyetembelea banda la WRRB.

Bw. Bangu amesema utaratibu huo utahakikisha matunda yanayovunwa ni yale tu yaliyofikia viwango vinavyohitajika na wanunuzi, jambo litakalopunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuhifadhi ubora wa bidhaa na kuongeza thamani ya biashara ya parachichi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Stakabadhi za Ghala Bw. Asangye Bangu akitoa ufafanuzi kuhusu ubunifu ulioanzishwa kwenye zao la parachichi na matunda mengine yenye soko kimataifa

Aidha, amesema WRRB inatarajia kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania ili kuunganisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na huduma za kidijitali za biashara pamoja na usafirishaji wa bidhaa.

Amesema ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa biashara, kurahisisha miamala na kuimarisha imani ya wanunuzi katika soko.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu Huduma wa WRRB, Bw. Mwita Thomas, amesema mfumo huo unaendelea kupanuliwa kutoka kwenye mazao ya kilimo pekee na sasa unahusisha pia bidhaa zisizo za kilimo, zikiwamo mifugo hai, mwani na samaki wanaofugwa kwenye vizimba.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *