Hotuba ya Mh. Makonda, Waziri wa Habari

MUHTASARI WA HOTUBA YA MHESHIMIWA PAUL CHRISTIAN MAKONDA (MB.), WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO, AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA
FEDHA 2026/27

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo iliyochambua Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika Bunge lako Tukufu, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (Fungu 96) kwa mwaka wa Fedha 2026/27.

Mheshimiwa Spika, naomba hotuba yangu yote iingie katika kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) kama ilivyowasilishwa.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupatia uhai, afya njema na kutuwezesha kukutana tena siku ya leo kujadili ustawi wa sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo. Tuendelee kumwomba Mwenyezi Mungu atuongoze katika kujadili hotuba hii ya bajeti kwa dhamira ya kuhakikisha Sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zinakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa unyenyekevu mkubwa nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kwanza, kuwa Naibu Waziri na baadaye Waziri kamili wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hii ni heshima kubwa sana kwangu na kwa familia yangu na naichukulia kama chachu ya kuendelea kulitumikia Taifa hili kwa bidii, weledi na uadilifu mkubwa. Ninamwahidi utumishi uliotukuka katika kuzisimamia sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo. Sekta hizi ni za kimageuzi, zikisimamiwa vizuri zitazalisha ajira kwa vijana. Hili litakuwa lengo langu katika kipindi chote nikiwa katika nafasi hii. Kama alivyosema Mheshimiwa Rais wakati ananiapisha, VIJANA TUNAELEWANA NA TUTAKWENDA PAMOJA.

Mheshimiwa Spika, niruhusu nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na maono mapana yanayolenga kuleta maendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla. Pia, nimpongezee kwa kuendelea kuliongoza Taifa vyema katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan migogoro ya vita ya Mashariki ya Kati na vita ya Urusi na Ukraine ambayo imeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa dunia, ikiwemo kupanda kwa bei za mafuta na bidhaa mbalimbali. Pamoja na changamoto hizo, Mheshimiwa Rais ameendelea kutuongoza kama Taifa kubaki katika umoja, mshikamano na amani.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Hotuba yake ya Bajeti iliyotoa utekelezaji wa malengo ya Serikali katika mwaka 2025/26 na mwelekeo wa shughuli za Serikali kwa mwaka 2026/27. Pamoja na masuala mengine hotuba hiyo imetoa maelezo kuhusu Sekta zilizo chini ya Wizara. Wizara yangu imezingatia na itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa.

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nikupongeze wewe Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuliongoza kwa busara na weledi mkubwa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maelekezo na miongozo yako imekuwa msingi wa ufanisi mkubwa wa Bunge katika kuisimamia Serikali kutekeleza vema majukumu yake. Vilevile, ninampongeza Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mb.), Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukusaidia na kukushauri vema katika majukumu yako ya kuliongoza Bunge. Nawapongeza sana Wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika (Mb.), Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso (Mb.) na Mheshimiwa Najima Murtaza Giga (Mb.) kwa kusimamia vema na kwa ustadi mkubwa mijadala katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, nichukuwe fursa hii kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko (Mb.), na Mheshimiwa Cornel Lucas Magembe (Mb.), Makamu Mwenyekiti wa Kamati pamoja na wajumbe wote wa Kamati kwa maelekezo, ushauri na maoni yao kwa Wizara yangu ambayo yametusaidia sana katika kuboresha utendaji kazi. Maelekezo yao yamesaidia kwa kiwango kikubwa katika uwasilishaji wa hotuba hii mbele ya Bunge lako Tukufu. Kamati hii imekuwa nguzo muhimu katika usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa bajeti na ukaguzi wa miradi, ambapo imefanikisha kuhakikisha rasilimali za umma zinatumiwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya umma. Kama misingi ya nyumba imara, ndivyo uongozi wa Kamati hii ulivyojenga msingi madhubuti wa maendeleo, unaoleta mafanikio endelevu na mabadiliko chanya katika jamii yetu.

Mheshimiwa Spika, ni masikitiko yangu kwamba katika kipindi cha mwaka 2025/26 Bunge lako Tukufu lilipatwa na misiba mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge. Misiba hiyo ni pamoja na msiba wa Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, aliyekuwa Mbunge wa Isimani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Jenista Joachim Mhagama aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Peramiho, na Mheshimiwa Halima Idd Nassor aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu akiwawakilisha Wafanyakazi. Kwa niaba ya Wizara na wadau wetu, tunatoa pole kwako Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, familia za marehemu, ndugu, jamaa na marafiki na Watanzania wote kwa ujumla. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote hiki ni kutokana na ushirikiano mzuri miongoni mwa wadau wa Wizara wakiwamo viongozi, watumishi, wadau na washirika wa maendeleo wa Wizara. Natambua mchango wao mkubwa wanaoutoa kwa Wizara ambao umeleta matunda ninayojivunia mbele ya Bunge lako Tukufu leo hii.

Mheshimiwa Spika, niruhusu kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru Mheshimiwa Hamis M. Mwinjuma (Mb.), Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Aidha, nimshukuru Bw. Gerson P. Msigwa, Katibu Mkuu; Bw. Methusela S. Ntonda, Naibu Katibu Mkuu; Wakuu wa Idara na Vitengo; Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara; na watumishi wote wanaofanya kazi kwa bidii na wanaohakikisha mipango ya Wizara inatekelezwa kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni mhimili kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla, ambayo kwa maneno mengine naweza kusema ni Wizara yenye nguvu shawishi (soft power) ya nchi inayobeba Taifa letu na kulitambulisha kwa Mataifa. Sekta ya habari imekuwa na mchango mkubwa katika kuhabarisha, kuelimisha, kuburudisha na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa muhimu zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi yetu. Aidha, utamaduni wetu ni uti wa mgongo wa Taifa letu. Hivyo, kupitia sekta ya utamaduni Serikali imeendelea kujenga uzalendo, kuhifadhi mila na desturi pamoja na maadili ya Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa sekta hizi hususan michezo imefanya uwekezaji mkubwa unaolenga kuinua Tanzania katika ramani ya michezo. Mheshimiwa Rais amewekeza zaidi ya shlingi trilioni 1.2 katika michezo ikiwa ni sehemu ya kuifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON 2027. Uwekezaji huo upo katika timu za Taifa, uendeshaji wa michezo pamoja na miundombinu ya michezo.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KWA KIPINDI CHA MWAKA 2025/26

MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA

Ukusanyaji wa Maduhuli
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ilikadiria kukusanya shilingi 1,036,000,000 ambapo hadi kufika mwezi Aprili 2026, shilingi 699,706,093, sawa na asilimia 67.5 ya lengo la mwaka zilikuwa zimekusanywa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, kiasi kilichokadiriwa kukusanywa ni shilingi 40,295,192,000, ambapo hadi mwezi Aprili 2026, shilingi 17,020,063,684, sawa na asilimia 42 ya lengo zilikuwa zimekusanywa.

Bajeti ya Wizara na Mtiririko wa Fedha

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara iliidhinishiwa bajeti yenye jumla ya shilingi 519,660,073,000. Kati ya fedha hizo, Mishahara ni shilingi 33,408,813,000, Matumizi Mengineyo ni shilingi 28,065,472,000 na Miradi ya Maendeleo ni shilingi 458,190,788,000.

Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Aprili 2026, Wizara ilikuwa imepokea jumla ya shilingi 352,942,454,472.97, sawa na asilimia 67.9 ya bajeti yote. Kati ya fedha zilizopokelewa, Mishahara ilikuwa shilingi 27,684,544,158.90, sawa na asilimia 82.9 ya bajeti ya Mishahara; Matumizi Mengineyo ni shilingi 20,925,566,233.81, sawa na asilimia 74.6 ya bajeti ya Matumizi Mengineyo; na Miradi ya Maendeleo ni shilingi 304,332,344,080.26, sawa na asilimia 66.4 ya bajeti ya Miradi ya Maendeleo.

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA 2025/26

SEKTA YA HABARI
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali imeendelea kuisemea Serikali kwa kutoa taarifa mbalimbali kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi Aprili 2026, Wizara imefanikiwa kuandaa mikutano 22 ya Msemaji Mkuu wa Serikali na vyombo vya Habari.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata taarifa sahihi kuhusu mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali, Wizara imeratibu mikutano 30 ya taasisi za Serikali kuzungumza na waandishi wa habari ambapo. Aidha, iliratibu mikutano 15 ya Waheshimiwa Mawaziri kuelezea utekelezaji wa majukumu na utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha siku 100 za muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita. Vilevile, Wizara imechapisha nakala 20,000 za Jarida la NCHI YETU linalohusu mafanikio ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TBC imeendelea na utekelezaji wa mradi wa Upanuzi wa Usikivu kwa kujenga vituo vya kurusha matangazo ya redio, masafa ya FM katika Wilaya 18 nchini. Ujenzi unaendelea katika Wilaya za Kalambo (Rukwa), Liwale (Lindi), Rufiji (Pwani), Biharamulo (Kagera), Urambo na Igunga (Tabora), Karatu (Manyara), Kilolo (Iringa), Ulanga (Morogoro), Iramba (Singida) na Ngara (Kagera). Wakati huo huo, TBC imepokea mitambo ya masafa ya FM kwa ajili ya Wilaya za Tanganyika (Katavi), Gairo (Morogoro), Hanang (Manyara), Siha (Kilimanjaro) na Mpwapwa (Dodoma). Aidha, TBC inashirikiana na wadau wengine wa maendeleo ya mawasiliano na teknolojia ya habari ikiwemo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambapo mradi wa upanuzi wa usikivu unatekelezwa katika Wilaya kumi (10) za Kyerwa (Kagera), Chunya (Mbeya), Kiteto (Manyara), Chemba (Dodoma) na Mkinga (Tanga). Maeneo mengine ambayo mradi unatekelezwa ni katika maeneo ya: Bukombe (Geita), Usangi (Kilimanjaro), Rombo (Kilimanjaro), Buhigwe (Kigoma) na Tunduru (Ruvuma).

Mheshimiwa Spika, TBC kwa kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inatekeleza mradi wa upanuzi wa usikivu katika Wilaya 15 na kazi ya ufungaji wa mitambo ya kurushia matangazo imekamilika kwenye vituo vya Arumeru (Arusha), Meatu (Simiyu), Sengerema (Mwanza), Kilosa (Morogoro), Mpwapwa (Dodoma) na Momba (Songwe). Aidha, ujenzi wa majengo ya kuhifadhi mitambo inaendelea kwenye halmashauri za Iringa Vijijini (Iringa), Lushoto (Tanga), Simanjiro (Manyara), Mpimbwe (Rukwa), Nyang’hwale (Geita), Kilombero (Morogoro), Nkasi Kusini (Rukwa), Itigi (Singida) na Mkalama (Singida).

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ujenzi wa vituo hivi kutaongeza usikivu hadi asilimia 98. Hadi Aprili 2026, usikivu wa redio za TBC umefikia Wilaya 139.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa TBC inawafikiwa vijana kwenye majukwaa ya mtandaoni maboresho makubwa ya kimaudhui na mifumo yamefanyika kupitia BongoFM, TBC2 na TBC Mtandao. Chaneli hizi za kimkakati zimekuwa chachu kwa kuongeza watazamaji, wafuatiliaji na wasikilizaji. Vilevile, TBC kupitia chaneli yake ya Tanzania Safari ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutangaza fursa za utalii na utajiri wa maliasili za nchi yetu imewezesha kuandaa maudhui na kutafsiri na kurusha jumla ya vipindi 1,125 katika lugha tano (5) za kimataifa ambazo ni Kireno, Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa na Kichina.

Mheshimiwa Spika, tarehe 2 Septemba, 2022 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa Bagamoyo kwa ajili ya maandalizi ya filamu ya ‘The Royal Tour’ aliagiza TANAPA kuitangaza njia ya utumwa kuwa kivutio cha Utalii. Kufuatia agizo hilo watalaamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kushirikiana na TANAPA walifanya utafiti na kuwasilisha ripoti iliyobainisha vivutio na mikakati ya utangazaji. Wizara kupitia TBC inatekeleza agizo hilo kwa kutambua njia misafara ya utumwa na wapagazi na kuitangaza kupitia Kampeni ya ‘The Slave Caravan’ inayorushwa na Chaneli ya Utalii ya Tanzania Safari. Kampeni hii inalenga kutangaza njia ya utumwa na vivutio vyake ambavyo havijulikani sana kwa watanzania na wageni. Kupitia kampeni hii vituo kumi na nne (14) vimebainishwa kutoka Zanzibar – Bagamoyo hadi Ujiji – Kigoma vitakavyotumika kuhifadhi historia ya watumwa, utumwa, masulia na maisha baada ya kukomeshwa kwa utumwa. Kupitia Kampeni hii ya ‘The Slave Caravan’, Serikali inatarajia kuigeuza historia chungu ya utumwa kuwa fursa ya elimu, uhifadhi na maendeleo ya utalii nchini Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Chaneli za TBC1, TBC2 na Tanzania Safari Chaneli kwa kupitia mtandao wa televisheni wa Canal+International zimeweza kufikia nchi 46 zinazoongea Kingereza, Kifaransa na Kireno. Nchi hizo ni pamoja na Angola, Benin, Burkina Faso, Botswana, Burundi, Kameruni, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Djibouti, Equatorial Guinea, Ethiopia, Eritrea, Eswatini, Gabon, Gambia, Ghana, Green Cape, Guinea Conakry, Guinea Bissau, Ivory Coast, Kenya, Liberia, Lesotho, Mali, Malawi, Mauritania, Mozambique, Namibia, Niger, Nigeria, Rwanda, Sao Tome, Senegal, Sierra Leone, Somalia, Sudani, Afrika Kusini, Sudani Kusini, Uganda, Tanzania, Togo, Zambia, Zimbabwe. Aidha, kupitia AZAM nchi saba (7) zimefikiwa ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi na Zimbambwe.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TSN imeendelea kutekeleza mradi wa ufungaji mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji kwa kujenga jengo la kiwanda cha uchapaji na kununua mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji. Hatua ya ujenzi wa jengo la kiwanda cha uchapaji imefikia asilimia 83.1. Ununuzi wa mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji umefikia asilimia 85.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TSN imeendelea kuboresha uandaaji na uchapaji wa maudhui kupitia Magazeti, Chaneli ya Mtandaoni na majukwaa ya mitandao ya kijamii. Maudhui hayo yalijikita katika kuhabarisha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hadi Aprili 2026, TSN imeandaa na kuchapisha jumla ya makala 2,973 za kimkakati.

Mheshimiwa Spika, TSN imeanzisha maktaba maalum ya historia kwa kuweka matoleo ya zamani ya magazeti na picha kwenye mfumo wa kidijiti. Jumla ya matoleo 12,600 ya Daily News na HabariLeo, picha 2,499 na makala maalumu 2,100 zimepatiwa alama ya utambuzi (indexing). Mfumu huu umehifadhi nyaraka zote muhimu zinazohusu historia ya nchi, historia kuhusu viongozi wakiwemo waasisi wa Taifa, historia ya harakati za ukombozi wa Uhuru kwa nchi za Kusini mwa Afrika na historia kuhusu masuala ya kidiplomasia. Kutokana na maktaba ya TSN kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu za kihistoria Kampuni imefanikiwa kuwa chanzo kikuu cha taarifa kwa ajili ya Kitabu cha Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa; Rais wa Awamu ya Pili, Hayati Ally Hassan Mwinyi; Kitabu cha Muungano; na picha zote zilizopamba Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere. Katika hatua ya uimarishaji wa mfumo wa kidigiti, kampuni imeunda mfumo wa TSN Intergreted Management Information System (TIMIS) unaounganisha Digital Archive na tovuti ya Kampuni ili kuwezesha kutoa huduma na kupata taarifa zote popote duniani.

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026 imepokea maombi na kusajili waandishi wa habari 4,139 kupitia mfumo wa Tai Habari ambapo Waandishi wa Habari 3,357 wenye vigezo vilivyoainishwa kwa mujibu wa sheria wamepatiwa ithibati. Malalamiko 14 ya uvunjifu wa maadili ya taaluma ya habari yameshughulikiwa.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imeandaa mwongozo maalumu wa kisheria utakaowezesha wanahabari wakongwe walioathiriwa na mfumo wa ithibati kurejea katika mfumo rasmi, kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 ambayo ilitungwa kwa ajili ya kukuza taaluma ya uandishi wa habari kwa kuweka mfumo wa kitaasisi utakaosimamia sekta ya habari. Mwongozo huu unaweka utaratibu wa kisheria wa kutambua na kuthibitisha umahiri wao kupitia tathmini maalumu ya uzoefu, weledi na maadili ya taaluma, na kuwawezesha kupata ithibati kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, kupitia ushirikiano kati ya Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuwawezesha vijana wanaojiajiri katika sekta ya habari kwa kuwawezesha mitaji ya kukuza, kuendeleza na kuzalisha kazi zao katika ubora unaokidhi mahitaji ya soko kupitia mikopo yenye masharti nafuu. Katika kutekeleza hayo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatoa shilingi 20,000,000,000 kwa ajili ya Mfuko wa Utamaduni na tayari 2,000,000,000 kwa ajili ya mikopo kwa Watengeneza Maudhui Mtandaoni (content creators) zimetoka kwa lengo la kuwasaidia kupata vitendea kazi na kuongeza uzalishaji wa kazi zao.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, imetoa mafunzo kwa watengeneza Maudhui Mtandaoni yenye lengo la kuwawezesha kutengeneza kazi zenye ubora kwa soko shindani la ndani na nje ya nchi. Mafunzo kwa awamu ya kwanza yametolewa kwa watengeneza Maudhui Mtandaoni 931 ambao kati yao wanawake ni 574 sawa na asilimia 62 na wanaume ni 357 sawa na asilimia 38 kutoka mikoa mitatu (3) ya Dar es Salaam (347), Mwanza (250) na Arusha (334).

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Maudhui imepewa jukumu la kusimamia maudhui yanayotolewa katika vyombo vya habari na kuchukua hatua pale kunapotokea ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na maadili. Kabla ya kuchukua hatua za kisheria, Serikali hutanguliza mazungumzo, ushauri na utoaji wa maelekezo kwa vyombo husika ikilenga kutoa fursa ya kujirekebisha. Hatua hizi huchukuliwa pale tu ambapo ukiukaji unaendelea, unajirudia au unasababisha madhara makubwa kwa umma. Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Wizara kupitia Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano imetekeleza majukumu yafuatayo:
Kufanya vikao tisa (9) vya Kamati vya kushughulikia mashauri dhidi ya watoa huduma 14 ambao walikiuka Sheria, Kanuni na Masharti ya Leseni zao;
Kufanya mapitio ya taarifa ya ukiukaji wa kanuni za utangazaji dhidi ya watoa huduma11 wa maudhui ya utangazaji waliobainika kuwa na ukiukaji wa mara kwa mara wa Sheria, Kanuni na Masharti ya Leseni; na
Kushiriki kwenye vikao vitatu (3) vya mashauriano na watoa huduma wa utangazaji wa maudhui kuhusu uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Masharti ya Leseni na Maadili ya Uandishi na Utangazaji wa Habari.

SEKTA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI

Mheshimiwa Spika, Tanzania imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa uanuai wa urithi wa utamaduni. Katika kuhakikisha kuwa urithi huu unalindwa, unahifadhiwa na kuendelezwa, Serikali imefanya utafiti wa kutambua, kuorodhesha na kulinda urithi wa utamaduni usioshikika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Utafiti huo uliofanyika kwa kushirikisha wadau wa utamaduni ulijikita katika kutambua na kuorodhesha Vazi la Kanga kama moja ya alama muhimu ya utambulisho wa Mtanzania na urithi wa utamaduni. Kufuatia utafiti huo, andiko la Vazi la Kanga liliwasilishwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa lengo la kuingizwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia wa Utamaduni Usioshikika inayosimamiwa na Shirika hilo. Manufaa ya kutambuliwa kwa urithi wa utamaduni wa Tanzania katika Orodha ya Urithi wa Dunia ni pamoja na kuongeza hadhi ya utambuzi wa kimataifa; kupata fursa za ufadhili wa uendelezaji na uhifadhi wa urithi huo kutoka kwenye mifuko ya kimataifa inayoratibiwa na UNESCO; kutangaza urithi wa utamaduni wa Tanzania pamoja na utalii wa kiutamaduni duniani.

Mheshimiwa Spika, jitihada nyingine zilizofanywa na Serikali kupitia Wizara ni kukamilisha uandaaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Kulinda Urithi wa Utamaduni Usioshikika (National Framework for Safeguarding Intangible Cultural Heritage). Katika kukabiliana na suala la mmomonyoko wa maadili nchini, umeandaliwa Mkakati wa Taifa wa kukabiliana na Mmomonyoko wa Maadili nchini. Mbali na mkakati huo, kupitia Televisheni ya Taifa TBC kimeanzishwa kipindi maalumu cha Maadili, Uzalendo na Utaifa kinachojulikana kwa jina la “Sisi ni Tanzania”. Kipindi hiki ni mahususi kwa ajili ya kuukumbusha umma wa Watanzania kuhusu umuhimu wa kurejea kwenye misingi ya maadili, mila, desturi, miiko, uzalendo na uadilifu.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha Kiswahili kinaendana na mabadiliko ya teknolojia, Wizara kupitia BAKITA imeandaa Kongoo ya Kiswahili ya Taifa (KOKITA). Kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, BAKITA imekusanya, imehariri na kuingiza maneno milioni 22 katika Kongoo ya Kiswahili ya Taifa (KOKITA), ambapo hadi Aprili 2026, kongoo hiyo ina jumla ya maneno milioni 61 na lengo ni kufikisha maneno milioni 100. Kongoo hii itakuwa daraja la kuongeza nafasi ya Kiswahili katika teknolojia ya kikompyuta hususani katika matumizi ya Akili Unde (AI). Pia Baraza linaendelea kukuza ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwamo Taasisi ya Mozilla ili kuwezesha kuimarisha Kiswahili katika Teknolojia.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia BAKITA imeongoza umma wa wazungumzaji wa Kiswahili, wadau na wapenzi wa Kiswahili Afrika na Duniani kote kushughudia hatua kubwa ya Kiswahili kukubalika kuwa lugha rasmi ya Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Kiswahili ni lugha ya kwanza ya Afrika kupata hadhi hiyo na hayo yalijiri katika Mkutano Mkuu wa 43 wa Shirika hilo uliofanyika Samarkand – Uzbekstani tarehe 30 Oktoba hadi 13 Novemba, 2025. Kwa muktadha huo, Kiswahili sasa ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendekleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika, Umoja wa Afrika, Umoja wa Wazalishaji Almasi Afrika na UNESCO. Vilevile, Kiswahili ni lugha pekee ya Afrika iliyotengewa siku ya kuadhimishwa ambayo ni tarehe 7 Julai kila mwaka. Katika hatua nyingine, Wizara kupitia BAKITA imefanya kikao na UNESCO pamoja na wadau wa maudhui ya mtandaoni kuhusu nafasi ya Kiswahili katika mitandao mikubwa ya kijamii ya META, TikTok na Google ili wapanue nafasi ya Kiswahili katika mitandao hiyo na hivyo kuongeza ajira na kipato kwa waandaaji wa maudhui kupitia mitandao ya kijamii.

Mheshimiwa Spika, katika kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, Serikali kupitia BAKITA inaendelea na shughuli ya usanifishaji wa Istilahi za michezo, ambapo hadi sasa jumla ya istilahi 420 za michezo zimesanifishwa.

Mheshimiwa Spika, Wahenga wanasema, “Asiyefahamu lugha, hafahamu mila”. Wizara kupitia BAKITA imeendelea kuuelimisha umma kuhusu kuzingatia matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu pamoja na utamaduni wake. Shughuli hii imehusisha kuandaa na kurusha hewani jumla ya vipindi 1,057 kupitia vituo vya redio na televisheni. Mafunzo ya msasa ya matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu pamoja na utamaduni wake yametolewa kwa Waandishi Waendesha Ofisi 844, Makatibu wa kamati za Halmashauri 12 pamoja na Wahudumu wa Mapokezi na Huduma kwa Wateja 52.

Mheshimiwa Spika, Baraza limeandaa na kufanya Kongamano la tano (5) la Idhaa zinazotangaza kwa Kiswahili Duniani likiwa na kaulimbiu “Tasnia ya Habari, Msingi wa Maendeleo ya Kiswahili Duniani”. Lengo kuu la Kongamano la Idhaa ni kuimarisha uhusiano wa taasisi za Kiswahili na vyombo vya habari ambavyo vinatekeleza jukumu kubwa la kukikuza na kukieneza Kiswahili ndani na nje ya nchi. Kongamano lilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha tarehe 24 hadi 27 Machi, 2026.

Mheshimiwa Spika, Tanzania ina jumla ya vituo 55 vya kufundisha Kiswahili kwa wageni, ambapo vituo 20 vipo nje ya nchi na 35 vipo nchini. Ufunguaji wa vituo hivi umeongeza chachu ya ujifunzaji wa Kiswahili kwa wageni.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika inaendelea kudumisha hadhi ya Tanzania kama “Mama wa Ukombozi wa Afrika” kwa vitendo, kwa kuhakikisha kuwa mchango wetu wa kihistoria unatambulika, unahifadhiwa na kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. Katika kuonesha dhamira hiyo, tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uamuzi wake wa kimkakati wa kuutekeleza mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kama ilivyoazimiwa na Umoja wa Afrika. Hatua hii inaakisi uongozi thabiti na dira ya kulinda historia ya Taifa letu huku tukiiweka katika nafasi ya kimataifa kama kitovu cha kumbukumbu za ukombozi wa Bara la Afrika.

Mheshimiwa Spika, katika hatua ya utekelezaji, Wizara kupitia Kituo imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 424.6 katika Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Uhifadhi wa Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kitakachokuwa Taasisi ya Umoja wa Afrika. Eneo hilo tayari limeshamilikishwa rasmi kwa Wizara, hatua inayoweka msingi imara wa utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati wa kitaifa na kibara.

SEKTA YA MAENDELEO YA SANAA

Mheshimiwa Spika, natoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake madhubuti na juhudi zake zilizopelekea kufanikisha Tanzania kupata heshima ya kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa zaidi ya ulimbwende duniani ya Miss World yatakayofanyika mwaka 2027. Mashindano haya yanatarajiwa kuleta manufaa makubwa kiuchumi na kijamii kupitia mapato ya viingilio, huduma za utalii, udhamini na biashara za wageni, pamoja na kutoa fursa kwa wabunifu wa ndani kujifunza na kujitangaza kimataifa. Aidha, tukio hili litasaidia kuitangaza Tanzania duniani kama kitovu cha utalii wa asili na utamaduni, kuimarisha diplomasia ya kimataifa na kuthibitisha usalama wa nchi kwa wageni. Mashindano ya Miss World Tanzania 2026 yalifanyika tarehe 19 Aprili, 2026 ambapo mlimbwende Latricia Ian Sawe aliibuka mshindi na ataiwakilisha Tanzania katika mashindano yatakayofanyika Vietnam mwezi Septemba 2026 ambapo Tanzania inatarajiwa kukabidhiwa rasmi bendera ya uenyeji kwa mwaka 2027. Mashindano ya Miss World 2027 yatatumika kama kichocheo cha hamasa kuelekea AFCON 2027 na kuongeza mwamko wa kitaifa pamoja na ushiriki wa wananchi katika maandalizi ya tukio hilo kubwa la kihistoria barani Afrika.

Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu Tamasha la CHAN-SINGELI lililofanyika tarehe 2 Agosti 2025 katika eneo la nje la Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni sehemu ya sherehe za uzinduzi wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa ligi za Ndani (CHAN 2024). Tamasha hili lilikuwa na mafanikio makubwa ambapo zaidi ya wasanii 30 wa muziki wa singeli walipata fursa ya kutumbuiza. Kupitia jukwaa hilo, Muziki wa singeli uliweza kutangazwa kimataifa kama sehemu ya utambulisho wa utamaduni wa Tanzania. Sambamba na hilo, Serikali imeendelea kuratibu Tamasha la Serengeti Music Festival, tamasha hili linatarajiwa kufanyika tarehe 30 Mei, 2026 linalenga kutumika kama jukwaa la kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mashindano ya AFCON 2027.

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Filamu Tanzania imeratibu Tamasha na Tuzo za Filamu (TAFFA). Tamasha hili lenye dhima ya ‘Filamu ni Biashara’ lililohusisha matukio kama midahalo, warsha na mafunzo kwa wadau wa filamu na michezo ya kuigiza lilifanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 03 Julai, hadi 16 Agosti, 2025 ambapo jumla ya wadau 1,600 walishiriki zikiwemo nchi za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Somalia, Uganda, Rwanda na Nchi kutoka nje ya Afrika ambazo ni Uswizi na Marekani. Tamasha hilo lilihitimishwa kupitia kilele cha usiku wa Tuzo za Filamu kilichofanyika tarehe 14 Februari, 2026 Jijini Dar es Salaam, ambapo jumla ya wadau 1,226 walishiriki. Jumla ya tuzo 28 zilitolewa katika tamasha hilo.

Mheshimiwa Spika, COSOTA iliendelea kufuatilia ukusanyaji wa tozo ya hakimiliki (Copyright Levy). COSOTA inaratibu mgao wa fedha zitokanazo na Tozo ya Hakimiliki ambapo jumla ya shilingi 988,656,103.92, sawa na asilimia 60 ya makusanyo yote ya shilingi 1,647,760,173.20 yaliyofanyika kuanzia Septemba 2023 hadi Juni 2025 zitagawiwa kwa wabunifu wa kazi za sanaa na uandishi. Mchanganuo wa mgao ni daraja la muziki asilimia 20, filamu asilimia 15, sanaa ya uandishi asilimia 10, sanaa za ufundi asilimia 7.5 na sanaa za maonesho asilimia 7.5.

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania umewezesha upatikanaji wa mikopo kwa wasanii kwa kushirikiana na Taasisi za Fedha. Serikali kupitia Mfuko imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.535 kwa miradi 229 ya Utamaduni na Sanaa. Aidha, Sekta zilizonufaika na mikopo hiyo ni Filamu (miradi 61) imewezeshwa shilingi 1,008,133,655.91, Ufundi (miradi 68) imewezeshwa shilingi 1,268,433,172.05; Maonesho (miradi 45) imewezeshwa shilingi 525,372,235.95, Muziki (miradi 44) imewezeshwa shilingi 433,060,936.09 na Lugha na Fasihi (miradi 11) imewezeshwa shilingi 300,000,000. Aidha, Miradi iliyowezeshwa imefikia Mikoa 15 ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Manyara, Arusha, Mwanza, Kagera, Shinyanga, Mara, Geita, Mbeya, Njombe, Kilimanjaro, Ruvuma, na Tabora. Halikadhalika, kupitia miradi iliyowezeshwa jumla ya ajira 75,537 zimezalishwa na kuwanufaisha wananchi 971,285.

SEKTA YA MAENDELEO YA MICHEZO

Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu kwa ufanisi michuano ya Mpira wa Miguu Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024). Mashindano ya CHAN ni kigezo ambacho Shirikisho la Soka Afrika (CAF) hutumia kama kipimo cha nchi kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON. Mashindano hayo yalifanyika nchini kuanzia tarehe 02 hadi 30 Agosti, 2025 ambapo nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zilikuwa wenyeji. Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ilishiriki na kuonesha kiwango cha juu cha ushindani kwa kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali, hatua inayodhihirisha kuimarika kwa soka letu la ndani. Aidha, kutokana na ubora wa maandalizi na usimamizi wa mashindano hayo CAF ilimtunuku tuzo ya heshima Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, sambamba na mashindano hayo, Serikali kupitia Wizara imeendelea na maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) kwa kutekeleza kwa ufanisi majukumu mbalimbali hususan ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo katika miji wenyeji ya Dar es Salaam Arusha ambayo ni: ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa umefikia asilimia 95; ukarabati wa viwanja vitatu (3) vya mazoezi vya Gymkhana, Meja Jenerali Isamuhyo na Shule ya Sheria umekamilika; ujenzi wa viwanja vitatu (3) vingine vya mazoezi vya Farasi, Leaders Club na Gymkhana II vipo katika hatua za awali; ujenzi wa uwanja wa Arusha wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 32,000 umefikia asilimia 77.5; na ujenzi wa kiwanja kimoja cha mazoezi kinachojengwa katika eneo la uwanja wa Arusha umefikia asilimia 60. Ni matarajio yetu kuwa kufikia Agosti 2026, Serikali itakamilisha miundombinu yote kwa ajili ya AFCON 2027.

Mheshimiwa Spika, katika kudhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali kuhakikisha tunafanikisha mashindano ya AFCON 2027, tayari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia na kutoa kiasi cha Dola za Marekani 30,000,000, sawa na shilingi 76,157,100,000 kama ada ya uandaaji wa mashindano husika. Hii ndiyo tafsiri halisi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mwanamichezo namba 1 nchini.

Mheshimiwa Spika, sambamba na maandalizi ya miundombinu ya AFCON 2027, Serikali imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu mingine ya michezo nchini kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati yenye lengo la kukuza vipaji na kuboresha huduma za michezo kwa wananchi. Miradi mingine ambayo inatekelezwa ni ujenzi wa Akademia ya Michezo katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 49, ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu jijini Dodoma wenye uwezo wa kuchukua watu 32,500 ambao umefikia asilimia 5, ujenzi wa Kituo cha Mazoezi na Kupumzikia Wananchi Jijini Dodoma ambao umefikia asilimia 73.5, ujenzi wa Kituo cha Mazoezi na Kupumzikia Wananchi jijini Dar es Salaam kilichofikia asilimia 49 na ukarabati wa uwanja wa Uhuru ambao umefikia asilimia 70.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imeendelea kuwezesha ushiriki wa wanamichezo na timu za taifa katika mashindano ya kimataifa. Serikali inampongeza mwanariadha Alphonce Felix Simbu aliyefanikiwa kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya riadha ya Dunia yaliyofanyika Septemba 2025 jijini Tokyo, Japani, ikiwa ni medali ya kwanza ya dhahabu kwa Tanzania katika mashindano hayo tangu kupata uhuru, pia kwa kuibuka mshindi wa pili na kushinda medali ya fedha katika mashindano ya marathoni ya kimataifa yaliyofanyika tarehe 20 Aprili, 2026 Jijini Boston, Marekani. Pia, tunampongeza mwanariadha John Nahhay Wele aliyetwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya nusu marathon yaliyofanyika tarehe 19 Aprili, 2026 nchini Poland.

Mheshimiwa Spika,, Serikali inazipongeza Timu ya Taifa ya mpira wa miguu “Taifa Stars” kwa kufika hatua ya 16 bora katika mashindano ya AFCON 2025 yaliyofanyika nchini Morocco na kufika hatua ya robo fainali ya mashindano ya CHAN 2024, Timu ya wanawake ya Futsal kwa kushiriki Kombe la Dunia 2025 nchini Ufilipino na kufika hatua ya makundi, “Twiga Stars” iliyotwaa ubingwa wa CECAFA Senior Women’s Championship 2025 na kufuzu WAFCON 2026, pamoja na timu ya mpira wa miguu kwa wenye ulemavu (amputee football) kwa kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati nchini Burundi. Aidha, Wizara inatoa pongezi kwa timu ya Taifa ya ngumi kwa kushinda jumla ya medali 18 (dhahabu 1, fedha 4 na shaba 13) katika mashindano ya kanda ya tatu Afrika yaliyofanyika Kenya mwaka 2025; timu ya mpira wa kikapu ya Dar City iliyoshiriki mashindano ya kikapu Afrika yaliyofanyika nchini Afrika Kusini na kufanikiwa kufuzu kucheza fainali ya mashindano hayo itakayofanyika nchini Rwanda Mei 2026; bondia Ibrahim Class alipigana na kuapata mikanda miwili ya WBC na WBO; bondia Lupakisyo Shoti alishinda mkanda wa IBO Afrika; Amani Bariki (Manichuga) alishinda mkanda wa WBC Intercontinental; Frank Shagembe alishinda mkanda wa WBO Afrika kwa uzito kg 90; Yusuph Changarawe ameshinda mkanda wa WBC Afrika; Halima Vunjabei alishinda mkanda wa PST, mafanikio hayo yanayoonesha maendeleo chanya ya michezo nchini.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia BMT kwa kushirikiana na Shirkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliratibu mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambao ulifanyika tarehe 13 Februari, 2026 jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliwaleta pamoja vigogo wa soka barani Afrika ukiwa na lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kukuza vipaji, kuimarisha ushindani wa vilabu na timu za Taifa, pamoja na kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya mpira wa miguu. Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni kielelezo cha uwezo wa nchi yetu kuandaa mikutano mikubwa na umeongezea hadhi ya Tanzania katika ramani ya soka Afrika hususan wakati mataifa yakijiandaa na fainali za AFCON 2027. Ujio wa viongozi hawa unaweka wazi kuwa nchi yetu inazidi kuaminiwa kama kitovu cha maamuzi makubwa ya michezo barani Afrika.

Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2025/26 yanapatikana katika ukurasa wa 13 hadi 148 wa kitabu cha hotuba yangu.

MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2026/27

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2026/27, Wizara na Taasisi zake kwa kushirikiana na wadau itatekeleza majukumu mbalimbali kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050; Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27 – 2030/31); Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2025 – 2030); Maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipohutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba, 2025; maelekezo ya Hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2026/27; Mpango Mkakati wa Wizara (2026/27 – 2030/31); Malengo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030; na Sera, Sheria na Miongozo mbalimbali ya Sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2026/27, Wizara imejipanga kutekeleza maeneo mbalimbali ya kipaumbele. Maeneo hayo ni pamoja na:
Kukamilisha kukarabati, kuboresha, kujenga na kuendelea kutunza miundombinu katika sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo;
Kukamilisha maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027 yatakayofanyika Juni hadi Julai 2027;
Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya 74 ya Urembo ya Dunia (Miss World);
Kukamilisha kutunga na kuhuisha Sera, Sheria, mikakati, miongozo na kanuni mbalimbali katika kuimarisha usimamizi na utekelezaji katika sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo;
Kuimarisha na kustawisha kiswahili kikanda na kimataifa;
Kuimarisha, kuziwezesha na kufanikisha ushiriki wa timu za Taifa katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa;
Kuboresha elimu na mafunzo katika tasnia za utamaduni, sanaa na michezo;
Kuweka na kuboresha mazingira wezeshi na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza na kuendeleza sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; na
Kuratibu, kuendesha na kusimamia matamasha, shughuli na matukio makubwa ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Spika, maeneo mahsusi yatakayopewa kipaumbele katika mwaka 2026/27 ni pamoja na: kuhakikisha upatikanaji wa maudhui ya redio (TBC) Taifa, Bongo FM na TBC International), Televisheni (TBC1, TBC2, Tanzania Safari Chaneli na Televisheni ya Kiingeraza), TBC mtandao, kurasa za mitandao ya Kijamii na redio za Kanda za TBC (TBC Dodoma na TBC Arusha); kuendelea kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha kwa kutangaza utekelezaji wa shughuli za kimkakati za Serikali; kuchapa na kusambaza nakala 1,909,752 za magazeti ya Daily News na HabariLEO; kuimarisha usimamizi wa uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kuboresha mifumo ya kupokea, kuchakata na kushughulikia malalamiko; kuendelea kutoa elimu kwa watoa huduma za kwa kuzingatia Kanuni, Miongozo, Masharti ya Leseni na Maadili ya Uandishi na Utangazaji wa Habari; kuratibu Kampeni ya kitaifa ya kukabiliana na changamoto za mmomonyoko wa maadili nchini; kuratibu Maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani katika ngazi ya kitaifa na kikanda ikiwemo kufanya Kongamano la Kimataifa la Kiswahili jijini Paris, Ufaransa; kusimamia uzingatiaji wa Maadili katika shughuli za Sanaa; na kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 20 kwa wadau 8,000 wa tasnia za habari, utamaduni na sanaa na ajira zinazotarajiwa kuzalishwa ni 105,000.

Mheshimiwa Spika, kuelekea mashindano ya AFCON 2027 yatayofanyika kuanzia tarehe 19 Juni hadi 17 Julai, 2027, Wizara imejipanga kikamilifu kwa kushirikisha wadau wote kuhakikisha mashindano haya siyo tu yanafanyika bali yanaweka historia na alama isiyofutika kwa taifa letu. Tayari tunazo Kamati mbalimbali za uratibu kitaifa na katika hili nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kitaifa na Waheshimiwa Mawaziri wote kwa ushiriki wao madhubuti.

Mheshimiwa Spika, pamaoja na miundombinu iliyoelezewa hapo awali, tayari Serikali imewaunganisha pamoja wadau katika sekta za utalii na ukarimu hususan mighahawa, hoteli na huduma za malazi, huduma za usafiri na ushafirishaji (magari, treni, ndege na meli), maeneo ya starehe na burudani kwa mashabiki (fun zones), maboresho ya muonekano wa miji yetu, vivutio vya utalii (mbuga, fukwe, malikale n.k.), matibabu ya kibingwa, ulinzi na usalama, uhamiaji n.k. Mkakati mahsusi wa hamasa kuelekea AFCON 2027 umeandaliwa ambapo utazinduliwa hivi karibuni na kuhakikisha kuwa kila mtanzania anakuwa sehemu ya mashindano haya kwa lengo lengo la kunufaika na fursa za AFCON na kutangaza nchi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hayo yote tumeendelea kushirikiana na wadau na wanamichezo maarufu walioonekana kusaidia au kutoa mchango mkubwa kwa nchi zao na dunia katika soka. Na hapa niruhusu nimtambue mwanamichezo maarufu Didier Drogba ambaye ni mchezaji bora wa wakati wote na nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Ivory Coast. Pia, amewahi kutumikia vilabu vikubwa vya mpira wa miguu duniani vya Chelsea na Galatasaray na ni mmiliki wa klabu ya Phoenix Rising ya Marekani. Uwepo wake leo ni uthibitisho tosha wa namna gani Serikali imeamua kuitumia AFCON 2027 kuitangaza taswira ya Tanzania kimataifa.

Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu mipango na bajeti ya Wizara kwa mwaka 2026/27 yanapatikana katika ukurasa wa 151 hadi 173 kitabu cha hotuba yangu.

About The Author