Joto la SGR lapanda Kasulu, Halmashauri kunufaika

Na. Mwandishi wetu – Kasulu

Halmashauri ya Mji Kasulu imeingia mkataba wa matumizi ya eneo la ardhi na Mkandarasi wa Ujenzi wa Reli ya Mwendo Kasi (SGR) kwa ajili ya uzalishaji wa matofali katika eneo lenye ukubwa wa ekali tano lililopo Shule ya Sekondari Kigoma Grand, Kata ya Msambala, Mtaa Mgongo.

Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo imefanyika jana katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Halmashauri hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Theresia Mtewele amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kufanikisha mradi huo huku akiwataka wakandarasi kushirikiana kwa ukaribu na Ofisi ya Mkurugenzi wanapokutana na changamoto mbalimbali ili kurahisisha utekelezaji wake.

“Matamanio yetu ni kuona shughuli hizi zinaenda vizuri, hivyo mtakapokumbana na changamoto yoyote mshirikiane na ofisi zetu ili tuweze kupata suluhisho kwa haraka” alisisitiza Mh. Mtewele

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ayubu Ngalaba amesema mradi huo utachochea maendeleo ya eneo hilo kwa kuwanufaisha zaidi wananchi kupitia kazi zitakazotolewa.

“Hatujachelewa, bado tupo kwenye muda sahihi wa kufaidika na fursa zinazotokana na mradi huu mhimu wa reli ya kisasa “SGR”

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mwl. Vumilia J. Simbeye ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza mradi huo ndani ya Halmashauri akiahidi kuonyesha ushirikiano mkubwa.

Kwa upande wa Mkandarasi wakiongozwa na mwakilishi wao Gan Baiwen wameishukuru Ofisi ya Mkurugenzi kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha kupatikana kwa eneo hilo.

Mradi huo unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa eneo husika.

Reli ya kisasa SGR itakayojengwa Kasulu ni sehemu ya kipande cha SGR kutoka Dar es Salaam hadi Burundi kinachojengwa kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Msongati mkoani Burunga nchini Burundi.

Uzinduzi wa ujenzi huo ulifanyika Musongati nchini Burundi mwaka 2025, huku serikali ya Burundi ikitangaza mkakati wa kuendrleza reli hiyo hadi mji mkuu wa Bujumbura na baadaye kuunganisha na nchi ya DRC.

About The Author