Kagame, Ruto kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi

Muktasari:

  • Ujio wa viongozi hao unatarajiwa kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha diplomasia ya kikanda na kuongeza ushawishi wake ndani ya Afrika Mashariki.

Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kuwapokea viongozi wawili wakuu wa Afrika Mashariki, hatua inayotajwa kuongeza wigo wa ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa katika ukanda huo.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Kenya, William Ruto wanatarajiwa kuwasili nchini kwa nyakati tofauti kati ya Mei 3 na 4, 2026.

Ziara hizo zinakuja wakati mataifa ya Afrika Mashariki yakiongeza juhudi za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kukuza biashara ya kikanda na kuendeleza mshikamano kupitia sera ya ujirani mwema.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais Kagame ataanza ziara yake ya kikazi Mei 3, 2026 na kupokewa rasmi na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kufanya mazungumzo ya faragha na ya pamoja yatakayolenga kuimarisha ushirikiano wa uwili katika sekta mbalimbali kabla ya kiongozi huyo wa Rwanda kurejea nyumbani.

Siku moja baadaye, Rais Ruto ataanza ziara ya kitaifa ya siku mbili kuanzia Mei 4 hadi 5, 2026, atapokelewa na mwenyeji wake Rais Samia katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, viongozi hao wanatarajiwa kushuhudia utiaji saini wa mikataba na makubaliano mbalimbali yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, uwekezaji na maendeleo ya pamoja na kisha kuzungumza na vyombo vya habari.

Aidha, Rais Ruto atashiriki katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Kenya, hatua inayotarajiwa kufungua fursa mpya kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa pande zote mbili.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kiongozi huyo pia atahutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma kabla ya kuhitimisha ziara yake.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Kenya umeendelea kuimarika, ambapo kati ya mwaka 2020 hadi 2024, biashara ya bidhaa kati ya nchi hizo ilichangia takribani asilimia 40 ya biashara yote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kwa upande wa Rwanda, ushirikiano wake na Tanzania umejengwa juu ya msingi wa kihistoria kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), huku biashara na uwekezaji vikiongezeka na kuchochea ajira kwa wananchi.

About The Author