Waandishi wa habari zaidi ya 3000 wapata ithibati

Bodi ya ithibati ya waandishi wa habari nchini Tanzania maarufu JAB imetajwa kupata mafanikio makubwa katika hatua za awali za uhakiki na usajili wa waandishi wa habari.

Mafanikio hayo yamethibitishwa leo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Paul Makonda wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma.

Mhe. Makonda, amesema kuanzia Julai 2025 hadi Aprili 2026, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imepokea na kushughulikia jumla ya maombi 4,139 ya usajili kupitia mfumo wa TAI HABARI.

Amebainisha kuwa kati ya maombi hayo, Waandishi wa Habari 3,357 waliokidhi vigezo vilivyoainishwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, wamepatiwa ithibati na kukabidhiwa vitambulisho vyao.

Waziri Makonda ameweka bayana kuwa pamoja na usajili huo, JAB imeshughulikia malalamiko 14 ya uvunjifu wa maadili ya taaluma ya habari, jambo linaloonesha kuanza kuimarika kwa mfumo wa uwajibikaji katika sekta hiyo.

Amsema kuwa sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016 ilitungwa kwa ajili ya kukuza taaluma ya uandishi wa habari kwa kuweka mfumo wa kitaasis utakaosimamia sekta ya habari.

“Mwongozo huu unaweka utaratibu wa kisheria wa kutambua na kuthibitisha umahiri wao kupitia tathmini maalumu ya uzoefu, weledi na maadili ya taaluma, na kuwawezesha kupata ithibati kwa mujibu wa sheria.” Alisema Mhe. Makonda

Hatua hii inalenga kulinda taaluma ya uandishi wa habari kwa kuhakikisha hata waandishi wa habari wenye uzoefu mkubwa wanapata nafasi ya kuingia katika mfumo rasmi unaotambuliwa kisheria.

Aidha, Mheshimiwa Makonda amesema Serikali kupitia JAB imeandaa mwongozo maalumu wa kisheria utakaowawezesha Waandishi wa Habari wakongwe walioathiriwa na mfumo wa ithibati kureiea katika mfumo rasmi, kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 ambayo ilitungwa kwa ajili ya kukuza taaluma ya uandishi wa habari.

Also Read  Rais Samia amteua Dkt Munisi Kuwa Naibu Waziri

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *