Muktasari:
- Mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya AMSONS Group ya Tanzania kwa mpango wa Sh90 bilioni kwa kushirikiana na Serikali ya Kenya
Dar es Salaam. Kenya inatarajia kujenga hospitali 10 za kisasa za mama na mtoto katika kaunti tisa chini ya makubaliano ambapo uwekezaji huo utagharimu thamani ya Sh90.75 bilioni (Ksh4.5 bilioni) yaliyosainiwa Aprili 29, 2026 katika Ikulu ya Nairobi, hatua inayolenga kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya mama na watoto wachanga.
Mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya AMSONS Group ya Tanzania kwa ushirikiano na Serikali ya Kenya, ambapo vituo hivyo vitajengwa katika kaunti za Nairobi, Kwale, Kisumu, Uasin Gishu na West Pokot.
Hospitali nyingine zitajengwa Mombasa, Garissa, Embu na Nakuru, huku Nairobi ikitarajiwa kuwa na hospitali mbili na kila kaunti iliyobaki kupata moja.
Maeneo hayo yalichaguliwa kulingana na mahitaji ya huduma za afya.
“Tumeingia ubia na AMSONS Group kuimarisha huduma za afya kwa mama na mtoto na kulinda maisha ya akina mama na watoto,” amesema Rais wa Kenya, Dk William Ruto, baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo.
Kila hospitali itakuwa na vitengo vya huduma za kabla ya kujifungua, vyumba vya uangalizi maalumu kwa akina mama (ICU), wodi za uchungu wa uzazi, kujifungua na uangalizi baada ya kujifungua, pamoja na angalau vyumba viwili vya upasuaji.
AMSONS Group itatoa vitanda 250 kwa ajili ya hospitali hizo, huku Serikali ikitoa vifaa vya ziada vya tiba na huduma za usaidizi.
Rais Ruto amesema Serikali pia inachunguza uwezekano wa ushirikiano zaidi ili kujenga hospitali nyingine 14 kama sehemu ya juhudi za kupanua upatikanaji wa huduma za afya, hasa katika maeneo ambayo hayajahudumiwa vya kutosha.
Mradi huo unalenga kusogeza karibu huduma maalumu za afya na kupunguza umbali mrefu ambao wajawazito hulazimika kusafiri kupata huduma za dharura za uzazi.
Katika maeneo mengi ya nchi, upungufu wa miundombinu, uhaba wa wataalamu na mapungufu katika utoaji wa huduma umeendelea kuhatarisha maisha ya akina mama na watoto wachanga.
Akielezea makubaliano hayo kuwa ni hatua muhimu katika kuziba pengo la huduma za afya kwa mama na mtoto, Rais Ruto amesema: “Leo tunachukua hatua madhubuti kubadilisha hali hii.”
Ameongeza kuwa mpango huo hauhusu miundombinu pekee, bali unalenga kujenga mfumo wa afya ulio sawa, uliounganishwa na unaoitikia mahitaji ya wananchi.
Akipongeza AMSONS Group kwa uwekezaji huo, Rais alisema unaendana na ajenda pana ya Serikali ya kuweka sekta ya afya katikati ya mabadiliko ya taifa.
“Tutaendelea kupanua upatikanaji wa huduma hizi hadi ziwafikie wote wanaozihitaji,” amesema, akibainisha kuwa kupunguza vifo vya akina mama na watoto ni kipaumbele cha kitaifa.
Amesema uwekezaji huo umefika kwa wakati muafaka, akisisitiza kuwa vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua bado ni vingi kupita kiasi.
“Akina mama na watoto wengi bado wanapoteza maisha hospitalini. Hili halikubaliki,” amesema.
Rais Ruto amethibitisha dhamira ya Serikali ya kukusanya rasilimali kwa Mfuko wa Huduma za Afya za Msingi na Mfuko wa Huduma za Dharura na Mahututi ili kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana na kumudu kwa wananchi wote.
Alisisitiza kuwa upatikanaji wa huduma bora za afya ni haki ya msingi na akatoa wito wa uwajibikaji wa pamoja katika kujenga, kuandaa, kuajiri na kuendesha hospitali hizo.
“Ni jukumu la pamoja kuhakikisha hospitali hizi zinaleta matokeo halisi kwa akina mama na watoto,” alisema.
Mpango huo unaendana na mkakati wa Kenya wa Huduma ya Afya kwa Wote (Universal Health Coverage), unaolenga kuimarisha mifumo ya huduma za afya za msingi.
Zaidi ya wahudumu 100,000 wa afya ya jamii, walioajiriwa na Serikali za kaunti na kuungwa mkono na Serikali za kitaifa na kaunti, wanatarajiwa kuwa na jukumu muhimu katika utambuzi wa mapema wa magonjwa, rufaa na ufuatiliaji wa huduma katika ngazi ya kaya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa AMSONS Group, Edha Nahdi amesema Kenya ni sehemu muhimu ya maono ya kampuni hiyo katika ukanda huu.
“Kwa AMSONS Group, Kenya si soko tu wala jirani, ni sehemu muhimu ya utambulisho wetu wa kikanda. Katika mwaka uliopita, tumepanua uwekezaji wetu nchini Kenya, ikiwemo ununuzi wa Bamburi Cement na East African Portland Cement. Tumepokelewa kwa mikono miwili, na tunashukuru serikali na wananchi wa Kenya,” alisema.
Amesema hatua ya kampuni kuingia katika sekta ya afya inaonyesha dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya jamii zaidi ya uwekezaji wa viwandani.
“Biashara yenye mafanikio ya kweli haijengi viwanda pekee inajenga jamii. Ukuaji wetu lazima uendane na ustawi wa watu tunaowahudumia. Leo, tunapanua wigo wetu kutoka miundombinu ya viwanda hadi miundombinu muhimu zaidi afya ya binadamu,” amesema.
Nahdi amesema mpango huo uliopewa jina la Mama na Mtoto Kwanza utalenga moja kwa moja huduma za afya kwa mama na mtoto.
“Chini ya mpango huu, AMSONS Group itajenga na kuandaa hospitali 10 za uzazi za Level 4 na hospitali moja ya Level 5, zote zikiwa zimebuniwa mahsusi kwa ajili ya mama na mtoto. Tumeona takwimu na kusikia simulizi za akina mama wanaosafiri umbali mrefu kutafuta huduma. Tupo hapa kusema kuwa hakuna mama anayepaswa kupoteza maisha wakati akileta uhai mpya,” amesema.
Ameongeza kuwa ujenzi unatarajiwa kuanza ndani ya siku 90 baada ya kukamilika kwa taratibu muhimu, huku hospitali hizo zikitarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo mwaka 2028.
“Zikikamilika, hospitali hizi zitahudumia angalau akina mama na watoto milioni moja kila mwaka. Zitajengwa kwa viwango vya kimataifa kama sehemu ya dhamira yetu ya ubora na uendelevu. Huu siyo ujenzi wa majengo pekee, bali ni kuacha urithi wa kudumu wa huduma,” amesema Nahdi.
