Na. Hafidhi Ally – RUJAT Iringa
Serikali Imeshauriwa kuongeza juhudi za kuwawezesha wajane na wagane kupata haki zao kwa wakati, hususan katika masuala ya mirathi na uwezeshaji wa kiuchumi baada ya kufiwa na wenza wao.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wajane yaliyofanyika kimkoa Juni 23, 2026 katika Shule ya Sekondari Kilolo, wilayani Kilolo, Afisa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la SOS Children’s Villages, Bi. Jesca Kawonga, alisema kuna umuhimu wa Serikali kutoa kipaumbele kwa wajane na wagane kwa kuwasaidia kupata mirathi kwa haraka pamoja na kuwawezesha kupata mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kuendelea kuhudumia familia zao.
Nao Baadhi ya wajane na wagane waliohudhuria maadhimisho hayo waliiomba Serikali kuharakisha upatikanaji wa haki za mirathi, wakieleza kuwa wamekuwa wakitumia muda mrefu mahakamani kufuatilia haki na mali walizoachiwa na wenza wao.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mh. Kheri James, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, amewataka wajane na wagane kujenga utamaduni wa kutenganisha mali za familia na mali za ndugu ili kuepusha migogoro na changamoto zinazoweza kujitokeza pindi mmoja wa wanandoa anapofariki dunia.
Maadhimisho ya Siku ya Wajane mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo: “Imarisha Haki, Utu na Uwezeshaji wa Kiuchumi.”






