Na. John Kabambala, RUJAT Morogoro
Tanzania imeingia katika hatua mpya ya kuendeleza biashara ya masoko ya kaboni, huku Serikali ikiweka mikakati ya kuifanya nchi kuwa miongoni mwa vinara wa soko hilo barani Afrika. Kupitia Jukwaa la Uwekezaji na Maendeleo ya Masoko ya Kaboni la mwaka 2026, lililoandaliwa na Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), Serikali iliweka wazi dhamira yake ya kujenga soko lenye uadilifu, uwazi na ushindani wa kimataifa, ambalo halitakuwa chanzo cha mapato ya taifa pekee, bali pia litachangia kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Jukwaa hilo lililofanyika mwishoni Mwezi Oktoba, 2026, katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro, liliandaliwa na NCMC chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Chama cha Waendelezaji wa Kaboni Tanzania (TaCaDevA), Ubalozi wa Ufalme wa Norway, Benki ya CRDB na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP). Lili wakutanisha takribani washiriki 200 katika vikao vya mchana na wengine 100 katika mapokezi ya jioni, wakiwemo viongozi wa Serikali, waendelezaji wa miradi ya kaboni, wawekezaji, taasisi za fedha, wataalamu, washirika wa maendeleo na wawakilishi wa mamlaka za serikali za mitaa.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Waziri Hamad Masauni alieleza dhamira ya Tanzania kuwa kitovu cha soko la kaboni lenye ubora na uadilifu ukanda wa Afrika Mashariki, kati na bara zima. Kuwa biashara ya kaboni inapaswa kutafsiriwa katika manufaa yanayoonekana kwa wananchi, ikiwemo ajira kwa vijana, mapato kwa vijiji, uwekezaji katika nishati safi na kuimarisha uhifadhi wa misitu. Serikali pia inalenga kuhakikisha kuwa fursa zinazotokana na biashara hiyo zinachangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 na kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika kuendeleza ajenda hiyo, Serikali imeweka lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Hatua hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa nishati zinazochangia uharibifu wa misitu na uchafuzi wa mazingira, huku ikifungua fursa za uwekezaji katika teknolojia za kupikia kwa kutumia nishati safi. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Waziri Masauni, uwekezaji katika sekta hii pamoja na miradi mingine ya kupunguza uzalishaji wa gesi joto unaweza kuiwezesha Tanzania kunufaika na mapato yatokanayo na uuzaji wa mikopo ya kaboni katika masoko ya kimataifa.

Hata hivyo, kufikia malengo hayo kunahitaji ushiriki wa sekta mbalimbali za uchumi. Serikali imezitaka taasisi za umma na mashirika ya serikali kuchangamkia fursa za biashara ya kaboni kwa kuingiza vipengele vya upunguzaji wa gesi joto katika miradi yao ya kimkakati. Taasisi zilizotajwa ni pamoja na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kupitia matumizi ya mabasi ya umeme na gesi, Shirika la Reli Tanzania (TRC), kupitia mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kupitia usambazaji wa majiko safi, na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kupitia miradi ya umeme wa maji na jua. Taasisi hizo zilitakiwa kuwasilisha mipango yao NCMC, huku Serikali ikitoa muda wa miezi sita kwa taasisi husika kujumuisha vipengele vya upunguzaji wa gesi joto katika miradi yao.
Ili kuimarisha utekelezaji, Serikali pia imeeleza kuwa imetenga zaidi ya shilingi bilioni tano (bn 5) katika bajeti ya mwaka husika kwa ajili ya kujenga na kuboresha mifumo ya kitaasisi pamoja na kuanzisha kanzidata ya taifa ya usajili wa miradi ya kaboni. Hatua hiyo inalenga kukamilisha miongozo ya Ibara ya Sita ya Mkataba wa Paris na taratibu za kimataifa, ikiwemo Mfumo wa Kimataifa wa Kufidia na Kupunguza Uzalishaji wa Kaboni katika Usafiri wa Anga (CORSIA). Serikali pia imeweka fursa ya upandaji wa miti bilioni mbili kila mwaka nchini kama sehemu ya juhudi za kuongeza uoto wa asili, kuhifadhi misitu na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.
Umuhimu wa hatua hizo unaongezeka kutokana na nafasi ya Tanzania katika rasilimali za asili zinazoweza kuendelezwa kupitia biashara ya kaboni. Tanzania ina takribani hekta milioni 43 za misitu, pamoja na maeneo makubwa ya mikoko, nyanda za malisho na mifumo mingine ya ikolojia. Rasilimali hizo zinaifanya nchi kuwa na nafasi kubwa ya kuendeleza miradi inayohusiana na uhifadhi wa misitu, urejeshaji wa maeneo yaliyoharibika, kilimo, nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu na kaboni ya bluu. Hii inaonyesha kuwa biashara ya kaboni nchini haiishii katika misitu pekee, bali inahusisha sekta mbalimbali zinazoweza kuchangia maendeleo ya uchumi wa kijani.
Kwa kutumia taarifa za rejista ya NCMC na rejista za kimataifa za kipindi cha Septemba hadi Oktoba 2026, zinaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa na maombi 117 ya miradi ya kaboni yaliyorekodiwa kwenye rejista ya NCMC, ambapo miradi 102 ilikuwa ikiendelea. Miradi hiyo inahusisha uhifadhi wa misitu na kupunguza uzalishaji unaotokana na uharibifu wa misitu (REDD+), upandaji na urejeshaji wa misitu (ARR), nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu, kilimo na kaboni ya bluu. Aidha, takribani miradi 70 ya Tanzania ilikuwa imeorodheshwa katika mifumo ya kimataifa ya Verra, Gold Standard na Plan Vivo, ambapo karibu miradi 35 ilikuwa imesajiliwa au kuthibitishwa na kuanza kufanya kazi.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa soko la kaboni nchini limeanza kuvuka hatua ya mipango na kuingia katika utekelezaji wenye matokeo yanayopimika. Awali miradi ya Tanzania ilikuwa imetoa zaidi ya mikopo milioni 10 ya kaboni hadi wakati wa kuandaa Makala hii. Mwaka 2026 pia ni mwaka wa rekodi, ambapo Verra pekee ilitoa mikopo milioni 4.1 ya kaboni kutoka kwenye miradi ya Tanzania, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya kiwango cha juu kilichowahi kurekodiwa katika mwaka mmoja uliopita. Hata hivyo, nyaraka hiyo inaeleza kuwa mafanikio ya kuendeleza miradi iliyopo kwenye maandalizi yatategemea maamuzi kuhusu upatikanaji wa fedha, utoaji wa vibali na namna ya kugawana manufaa na jamii.
Akifafanua kuhusu nafasi ya Serikali katika kuimarisha sekta hiyo, Katibu Mkuu wa wilzara ya hiyo Dkt. Richard Muyungi alieleza kuwa biashara ya kaboni imepata msukumo mkubwa tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Paris mwaka 2015, ambao uliweka msingi wa ushirikiano wa kimataifa katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi. Alibainisha kuwa Tanzania ina nafasi ya kuvutia mitaji, teknolojia na utaalamu kupitia soko hilo, lakini mafanikio yake yanategemea kuwepo kwa mifumo imara ya kitaalamu, kisheria na kifedha. Kwa mujibu wa maelezo yake, Serikali ina jukumu la kuweka mazingira wezeshi kupitia sera, sheria na taasisi zinazoweza kusimamia miradi, kuthibitisha matokeo na kuhakikisha kuwa shughuli zote zinafanyika kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Kwa muktadha huo, Dkt. Muyungi alieleza umuhimu wa marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira yaliyofanyika mwaka 2025 pamoja na kanuni za biashara ya kaboni za mwaka 2022 na marekebisho yake ya mwaka 2023. Mifumo hiyo imeweka msingi wa kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni na kuipa NCMC jukumu la kusimamia rejista ya taifa pamoja na mfumo wa Upimaji, Utoaji Taarifa na Uhakiki (MRV). Mfumo huo ni muhimu katika kufuatilia kiwango cha upunguzaji wa gesi chafuzi kinachotokana na mradi, kuripoti matokeo na kuyathibitisha kwa kutumia taratibu zinazokubalika. Uwepo wa mfumo huo unatarajiwa kuongeza uwazi, kuaminika kwa mikopo ya kaboni na uwezo wa Tanzania kushiriki katika masoko ya kimataifa.
Moja ya hatua muhimu zilizotajwa katika Concept Note ni utekelezaji wa programu ya MRV4TZ, inayoungwa mkono kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Norway na UNDP. Programu hiyo inalenga kuwezesha Tanzania kuwa na mfumo wa kidijitali wa usajili wa miradi ya kaboni na upimaji, utoaji taarifa na uhakiki unaokidhi viwango vya kimataifa. Uzinduzi wake uliwekwa kuwa sehemu muhimu ya Jukwaa la Uwekezaji na Maendeleo ya Masoko ya Kaboni la mwaka 2026. Mfumo huo unatarajiwa kusaidia NCMC kufuatilia miradi kwa ufanisi, kuboresha upatikanaji wa taarifa na kuwapa wawekezaji uhakika kuhusu hali na matokeo ya miradi inayosimamiwa nchini.
Kwa upande wa masoko ya kimataifa, Tanzania imekuwa ikijiandaa kushiriki katika mifumo ya biashara ya kaboni inayohusisha Ibara ya Sita ya Mkataba wa Paris na CORSIA. Hata hivyo Tanzania ilisaini vibali vyake vya kwanza vya Ibara ya Sita mwezi Agosti 2026 na kwamba mikopo ya kwanza yenye alama ya kuidhinishwa chini ya Ibara hiyo ilikuwa imetolewa. Hii inaashiria hatua muhimu katika ushiriki wa Tanzania katika soko la kimataifa la kaboni. Aidha, kupitia CORSIA, iliyoanzishwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) mwaka 2016, mashirika ya ndege yanaweza kutumia mikopo inayokubalika ya kaboni kufidia sehemu ya uzalishaji wao. Tanzania pia inaangalia uwezekano wa kuimarisha ushiriki wake katika sekta ya usafirishaji wa majini kupitia ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO).
CHANGAMOTO ZINAZO IKABILI NCMC.
Hata hivyo, kuongezeka kwa idadi ya miradi na mikopo ya kaboni hakumaanishi kuwa sekta hiyo haina changamoto. Akizungumza kwa niaba ya NCMC, Kathryn Kigaraba alieleza kuwa Tanzania inahitaji kuendelea kujenga mifumo madhubuti ya usajili, kuongeza utaalamu wa ndani wa kuhakiki na kuthibitisha miradi, na kuhakikisha kuwa wawekezaji pamoja na waendelezaji wanaelewa taratibu zinazotakiwa. Alisisitiza kuwa soko hilo linahitaji kuaminiana, uwazi na uelewa wa pamoja ili kuvutia uwekezaji wa muda mrefu. Kwa mtazamo huo, jukwaa lililofanyika Dar es Salaam lilikuwa fursa ya kuwakutanisha Serikali, waendelezaji wa miradi, taasisi za fedha, wawekezaji na washirika wa maendeleo katika kujadili changamoto na kutafuta suluhu za pamoja.
Kuna changamoto kuu nne zilizo ainishwa zinazohitaji kushughulikiwa ili kuimarisha soko hilo. Changamoto ya kwanza ni kutokuwepo kwa uelewa unaofanana kuhusu Ibara ya Sita ya Mkataba wa Paris, hasa masharti ya utoaji wa vibali, marekebisho yanayohusiana na uhasibu wa mikopo ya kaboni na muda wa kuripoti taarifa. Changamoto ya pili ni namna ya kupanga mgawanyo wa manufaa kati ya waendelezaji wa miradi, jamii na mamlaka za serikali za mitaa. Changamoto ya tatu ni tofauti kati ya matarajio ya wawekezaji na maandalizi ya waendelezaji wa miradi, hasa kuhusu masharti ya tathmini na uhakiki wa uwekezaji. Changamoto ya nne ni utayari wa kiutendaji wa rejista ya taifa na mfumo wa MRV, unaohitaji kueleweka kwa wadau wote ili waweze kujua huduma zilizopo na maboresho yanayotarajiwa kupitia MRV4TZ.
Katika kulijibu suala hilo, Kigaraba alibainisha kuwa NCMC inalenga kuanzisha mfumo jumuishi wa usajili wa kitaifa unaoendana na viwango vya kimataifa, pamoja na kukuza utaalamu wa Watanzania katika timu za uhakiki na uthibitisho wa miradi. Alieleza kuwa ni muhimu Tanzania kujenga uwezo wa ndani wa kusimamia soko lake badala ya kutegemea utaalamu kutoka nje pekee. Aidha, alitaja umuhimu wa kuunganisha mifumo mbalimbali ya kifedha, ikiwemo fedha za maandalizi ya miradi, fedha mchanganyiko, dhamana na mikopo yenye masharti nafuu, ili kusaidia miradi kuanzia hatua za awali hadi kufikia uwekezaji na utekelezaji. Hatua hiyo inatarajiwa kupunguza vikwazo vya kifedha na kuongeza uwezekano wa miradi ya kaboni kuwa endelevu na yenye uwezo wa kuvutia mitaji.
Kigaraba alieleza kuwa NCMC imeweka vipaumbele vitano vya maendeleo ya soko la kaboni. Vipaumbele hivyo ni kuandaa miradi imara ya kaboni, kuhamasisha mtaji wa ndani na wa kimataifa, kuimarisha uadilifu na uzingatiaji wa sheria, kupanua fursa za kushiriki katika masoko ya kimataifa, na kuhakikisha kuwa manufaa yanayotokana na biashara hiyo yanagawanywa kwa usawa. Alisisitiza kuwa uadilifu wa soko na maendeleo ya waendelezaji wa miradi havipaswi kuonekana kama mambo yanayokinzana. Badala yake, mfumo unaoaminika ndio utakaowezesha miradi kupata uwekezaji wa muda mrefu na kulinda thamani ya mikopo ya kaboni inayozalishwa nchini.
Suala la ushiriki wa jamii na mgawanyo wa manufaa limepewa nafasi muhimu katika mkakati huo. Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya miradi ya kaboni inayotegemea uhifadhi wa misitu na rasilimali za asili inahitaji ushirikiano wa wananchi wanaoishi katika maeneo husika.
Dkt. Albina Andrew Chuwa, Mjumbe wa Bodi, alieleza kuwa biashara ya kaboni ni fursa muhimu ya kiuchumi kwa Tanzania, hasa katika kipindi ambacho idadi ya watu inaongezeka na mahitaji ya fursa mpya za kipato yanaendelea kuongezeka. Alibainisha kuwa biashara hiyo inaweza kusaidia kuimarisha uchumi wa wananchi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, endapo manufaa yake yatafika kwa wananchi wanaoshiriki katika uhifadhi wa mazingira.
Dkt. Chuwa pia alieleza kuhusu fursa kubwa iliyopo katika kaboni ya bluu, inayohusishwa na mifumo ya ikolojia ya baharini na maeneo ya pwani, hususan misitu ya mikoko. Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, Tanzania ina takribani hekta 174,488 za mikoko, ambapo hekta 158,000 zipo Tanzania Bara na hekta 16,488 zipo Zanzibar. Alieleza kuwa mikopo ya kaboni inayotokana na maeneo ya mikoko inaweza kufikia hadi dola 60 za Marekani kwa mkopo, ikilinganishwa na dola 12 kwa mikopo inayotokana na miti ya kawaida. Rasilimali hizi zinaipa Tanzania nafasi ya kuendeleza uwekezaji unaounganisha uhifadhi wa mazingira ya baharini na manufaa ya kiuchumi, huku zikichangia lengo la kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kwa asilimia 30 hadi 35 ifikapo mwaka 2030 chini ya mpango wa NDC2.
Pamoja na fursa hizo, kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa mapato yanayotokana na biashara ya kaboni yanachangia maendeleo ya huduma za kijamii na ustawi wa wananchi. Dkt. Chuwa alitolea mfano Mkoa wa Kigoma, ambao kwa mujibu wa maelezo yake umepata takribani shilingi milioni 700 zilizotumika katika ujenzi wa shule na kuboresha huduma za afya. Pia alitaja Djibouti, Ghana, Gabon na Kenya kama mifano ya nchi zinazotumia mapato yanayotokana na kaboni kuimarisha sekta za elimu, afya na miundombinu. Alieleza kuwa bodi imeweka mpango mkakati wa miaka mitano unaohusisha mikutano ya kila baada ya miezi mitatu na sekta binafsi pamoja na wananchi wa vijijini wanaoshiriki katika uhifadhi wa misitu, ili kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha kuwa manufaa yanawafikia wahusika.
Kwa upande wa uwekezaji, ushiriki wa taasisi za fedha za ndani na nje umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya soko la kaboni. CRDB Bank imekuwa kiungo muhimu kushiriki katika kuunganisha fedha za ndani na miradi ya kaboni, huku wawekezaji na taasisi za kifedha za kimataifa wakitarajiwa kutoa mitaji na utaalamu. Jukwaa hilo pia lililenga kuwezesha waendelezaji wa miradi kukutana moja kwa moja na wawekezaji ili kuelewa mahitaji ya uwekezaji, masharti ya tathmini na namna ya kuandaa miradi inayoweza kufadhiliwa. Kupitia mikutano hiyo, NCMC ilitarajia kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kufungua njia mpya za upatikanaji wa fedha kwa miradi ya uhifadhi wa mazingira, nishati safi na nishati jadidifu.
Ushirikiano wa kimataifa nao umeendelea kuwa sehemu muhimu ya safari ya Tanzania katika kuendeleza soko hilo. Ubalozi wa Norway na UNDP umetajwa kuwa miongoni mwa washirika waliotoa mchango mkubwa katika kujenga uwezo, kuendeleza sera na kuandaa mazingira ya Tanzania kushiriki katika masoko ya kimataifa. Norway na UNDP pia zinashirikiana kufadhili programu ya MRV4TZ, wakati Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na NCMC ikiendelea kuweka mifumo ya usimamizi. Kwa upande mwingine, TaCaDevA inawakilisha waendelezaji wa miradi ya kaboni na kuchangia kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi. Ushirikiano huo unaonyesha kuwa mafanikio ya soko la kaboni yanahitaji nguvu ya pamoja ya Serikali, jamii, wawekezaji, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo.






