Na. Clement Robert, WAF – Dodoma
Serikali inapanga kuendelea na mradi wa ujenzi na uboreshaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuongeza uwezo wa utoaji huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini, hatua hiyo inalenga kuwezesha zaidi ya wataalam 4,000 waliopo Hospitalini hapo kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Hayo yamebainishwa leo Mei 9, 2026 Jijini Dodoma na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa katika semina ya Wabunge akibainisha kuwa pamoja na ujenzi wa hospitali mpya, bado Muhimbili ni nguzo muhimu ya huduma za afya, mafunzo ya wataalam pamoja na maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Amesema sababu kuu ya kuiboresha na kuijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili ni kuongezeka kwa mahitaji ya huduma na uchakavu wa majengo na miundombinu
“Tunatambua umuhimu wa kujenga hospitali mpya nchini, lakini bado Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ina nafasi kubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi. Ndiyo maana Serikali inaendelea na mradi wa ujenzi na uboreshaji wa hospitali hiyo ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya huduma, kuboresha mazingira ya kazi kwa wataalam wetu zaidi ya 4,000 na kuendana na hali ya uchakavu wa miundombinu iliyopo,” amesema mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa amesema Mwaka 2025 pekee, Hospitali ya Taifa Muhimbili ilihudumia wagonjwa 44,549 waliolazwa na wagonjwa wa nje 458,474, huku hospitali ikitumia kati ya shilingi bilioni 6 hadi 8 kila mwaka kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya miundombinu na vifaa, hali ambayo inapunguza uwezo wa kuelekeza rasilimali hizo katika dawa, vifaa tiba, na kuboresha huduma kwa wagonjwa

Aidha,utekelezaji wa Mradi huu unatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa gharama ya dola za Kimarekani USD 468,469,000, sawa na takribani Shilingi trilioni 1.2 za Kitanzania huku Kati ya fedha hizo, takribani dola za Kimarekani USD 363.9 milioni ni mkopo kutoka Korea Kusini, na USD 104.572 milioni ni mchango wa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kodi, maandalizi ya eneo la mradi, na gharama nyingine zinazobebwa na Serikali.
Mradi wa Muhimbili una gharama ya takribani dola 1,819 kwa mita ya mraba. Katika miradi yote iliyolinganishwa, kiwango hiki kinaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazolipa gharama ya chini zaidi. Kwa maneno mengine, hatupo kwenye kundi la miradi ya bei ya juu; tupo kwenye kundi la miradi ya gharama nafuu kwa kulinganisha na ukubwa na aina ya uwekezaji unaofanyika.
Mradi wa Muhimbili unakadiriwa kuwa na ukubwa wa takribani mita za mraba 115,000 ikiwa ni ukubwa unaozidi Hospitali nyingi katika nchi nyingine, zikiwemo baadhi ya nchi zenye uchumi mkubwa na mifumo ya afya iliyoendelea zaidi jambo linaloifanya Tanzania kuwa na hospitali kubwa, ya viwango, kwa gharama ya chini tofauti na nchi nyingi nyingine.






