Na Deogratius Temba, na Tamali Vullu
Matumizi ya jani la “sale” katika jamii ya Wachaga mkoani Kilimanjaro yameendelea kutajwa kuwa moja ya mila zinazochochea na kuficha vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku baadhi ya wananchi wakidai kuwa utaratibu huo wa kuombana msamaha umegeuka kinga ya watuhumiwa wa ubakaji na unyanyasaji wa watoto.
Tuhuma hizo zimeibuliwa na wananchi pamoja na wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia mradi wa kuimarisha mifumo ya jamii katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kulinda haki za wanawake na watoto, yaliyofanyika katika maeneo ya Mabogini (Moshi DC), Kalenga (Iringa DC) na Mgagao (Mwanga DC).
Washiriki wa mafunzo hayo wamesema mila ya kutumia jani la “sale” pamoja na “ngiambii”, jani dogo linalotambaa ardhini linalotumika kuashiria kuombana msamaha katika jamii ya Kichaga, imekuwa ikitumiwa vibaya kumaliza kesi za ukatili wa kijinsia nje ya mfumo wa sheria.
Mchungaji wa Kanisa la TAG, Mabogini, Lidyia Materu, amesema awali mila hiyo ilikuwa sehemu ya maridhiano ya kifamilia katika migogoro ya kawaida, lakini sasa imeanza kutumika hata kwenye makosa ya jinai, ikiwemo ubakaji na ukatili dhidi ya watoto.
“Mila hii imekuwa hatari sana kwa sababu watu wanaamini wataomba msamaha na suala litakwisha. Unakuta mtuhumiwa ameshakamatwa, lakini kesho yake familia zote zimekaa pamoja zinakunywa mbege, jani la sale linawekwa pembeni, halafu wanaambiwa ‘tumeshapatana’,” alisema.
Kwa mujibu wa wananchi wa jamii ya Wachaga, matumizi ya mila hiyo yamechangia familia nyingi kushindwa kufikisha kesi kwenye vyombo vya sheria, kutokana na hofu ya kuvunja mshikamano wa kifamilia na kijamii.
Mila na ukimya wa jamii
Wakati mjadala huo ukiendelea, wananchi wamekiri kuwa jamii yenyewe imekuwa sehemu ya tatizo kwa kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhalalisha baadhi ya tabia kandamizi kupitia mila na desturi.
Mjumbe wa Kamati ya Mtakuwwa Kata ya Mabogini, Elizabeth Chuwa, amesema jamii imefikia hatua ya kuona udhalilishaji wa wanawake kama jambo la kawaida.
“Unaweza kuona vijana wakimdhalilisha mwanamke barabarani na watu wote wanakaa kimya. Hakuna anayekemea kwa sababu jamii imezoea,” amesema.
Ameongeza kuwa hali hiyo imejenga mazingira ya ukimya hata kwa makosa makubwa kama ubakaji wa watoto.
“Mtoto anabakwa, lakini jamii inanyamaza. Watu wanaona ni jambo la kifamilia badala ya kosa la jinai,” amesema.
Uchambuzi wa wadau umeonesha kuwa baadhi ya mila ambazo hapo awali zilikuwa na lengo la kuleta maridhiano ndani ya jamii, sasa zimekuwa zikikinzana na sheria za kisasa na haki za binadamu, hususan pale zinapotumika kuficha uhalifu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA), makosa ya ukatili wa kijinsia ni ya jinai na hayawezi kumalizwa kwa maridhiano ya kifamilia au kimila.
Aidha, Tanzania ni mwanachama wa mikataba ya kimataifa ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) na Mkataba wa Haki za Mtoto, unaoelekeza jamii kuhakikisha wanawake na watoto wanalindwa dhidi ya ukatili.
Maridhiano yanayotajwa kuficha uhalifu
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro, Wakili Bora Mfinanga, amesema baadhi ya maridhiano ya kimila yanaambatana na vitendo vya rushwa.
“Haiwezekani mtu apewe pombe, fedha au mifugo halafu ikaelezwa kuwa ni msamaha wa kimila. Huo ni mchakato unaozuia haki,” amesema.
Amesisitiza kuwa sheria za Tanzania haziruhusu kesi za ubakaji au ukatili dhidi ya watoto kumalizwa kwa makubaliano ya kifamilia.
Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Jinsia Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, SP Asia Matauka, amesema jamii ina wajibu wa kutoa taarifa mapema badala ya kuficha matukio kwa kisingizio cha mila.
“Kesi za ukatili wa kijinsia hazipaswi kunyamaziwa wala kumaliziwa nyumbani. Manusura wanapaswa kulindwa na kupewa haki zao,” amesema.
Watoto, wasichana wazidi kuwa hatarini
Katika majadiliano ya jamii ya Kata ya Mabogini, imeelezwa kuwa ukimya wa jamii umechangia watoto wengi kubaki katika mazingira hatarishi, huku baadhi ya wazazi wakihofia aibu na hivyo kushindwa kutoa taarifa.
Katika Kata ya Mabogini na Tarafa ya Kibosho kwa ujumla, matukio mbalimbali ya ubakaji na unyanyasaji wa watoto yalitajwa kuhusisha watu wanaofahamika ndani ya jamii, lakini hatua zinadaiwa kutokuchukuliwa ipasavyo. Aidha, baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa wamedaiwa kuachiwa huru bila hatua madhubuti kuchukuliwa.
Vilevile, viongozi wa jamii wamekosoa kuongezeka kwa vilabu vya pombe za kienyeji na baa holela, hali inayotajwa kuongeza mazingira ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kiongozi mmoja wa kijiji cha Chekereni, ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema watoto wengi wameathirika kutokana na kuishi karibu na mazingira ya ulevi na biashara ya ngono.
“Watoto wanaona kila kitu hadharani. Wapo vilabuni hadi usiku, na jamii imekaa kimya kana kwamba ni kawaida,” alisema.
Ofisa ustawi wa jamii wa Kata ya Mabogini, Kunti Hutta, amesema suala la ulinzi wa watoto linahitaji ushirikiano wa jamii nzima.
“Wasichana wengi wanabaki mitaani hadi usiku baada ya masomo. Lazima wazazi, shule na jamii kwa ujumla wawajibike kuhakikisha wanakuwa salama,” amesema.
Wito wa kubadili mila zinazoumiza jamii
Mwezeshaji wa mafunzo kutoka TGNP, Deogratius Koyanga, amesema jamii ina wajibu wa kuchambua mila zake ili kuona zipi zinafaa kuendelea na zipi zinapaswa kubadilishwa kwa maslahi ya haki na usalama wa wanawake na watoto.
“Mila ni sehemu ya utamaduni wetu, lakini hazipaswi kutumika kuzuia haki. Jamii lazima ikubali kujadili kwa uwazi mila zinazochochea ukatili wa kijinsia,” amesema.
Kauli za wadau wanaotekeleza mnyororo wa kutokomeza ukatili wa kijinsia zinaonesha kuwa vita dhidi ya ukatili wa kijinsia haviwezi kufanikiwa bila jamii yenyewe kubadilika. Wadau wanaamini kuwa kuendelea kutumia mila kama jani la “sale” kuficha makosa ya jinai kunadhoofisha sheria, kunyamazisha waathirika na kuendeleza mzunguko wa ukatili katika jamii.






