Wizara ya Afya yajivunia matokeo chanya kupunguza vifo vya mama na watoto

Na. Shaban Juma, WAF – Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, kwa lengo la kupunguza na kukomesha vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama wajawazito na watoto wachanga nchini.

Dkt. Samizi amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Afya mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI   kuhusu hali ya vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga pamoja na mikakati ya Serikali ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Amesema Serikali inaendelea kuweka jitihada kuhakikisha mama mjamzito anapata huduma bora na kwa wakati kuanzia kipindi cha ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, huku huduma kwa watoto wachanga zikiendelea kupewa kipaumbele ili kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika.

Dkt. Samizi amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali zinahusisha kuimarisha miundombinu ya huduma za afya ya uzazi na watoto wachanga, kuongeza vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma za dharura za uzazi na mtoto, pamoja na kuongeza na kuboresha Wodi Maalum za Watoto Wachanga (NCU) katika hospitali mbalimbali nchini.

Dkt. Samizi akitoa taarifa ya Wizara kwa Kamati ya Bunge

Aidha, Dkt. Samizi amesema Serikali imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba muhimu kwa ajili ya huduma za watoto wachanga, hususan watoto wanaozaliwa kabla ya wakati au wenye changamoto za kupumua, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa oksijeni na huduma nyingine muhimu za kuokoa maisha.

Amesema, Serikali pia imeendelea kuongeza wataalamu wenye ujuzi katika huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma ili waweze kutambua mapema viashiria vya hatari na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.

Also Read  Ndejembi awasili Shinyanga kwa ziara ya kikazi, asisitiza uwajibikaji

Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amesema mfumo wa M-MAMA umeendelea kuimarisha huduma ya usafirishaji wa haraka wa wajawazito na watoto wanaohitaji huduma za dharura, hatua inayosaidia kupunguza ucheleweshaji wa kuwafikisha wagonjwa kutoka nyumbani kwenda vituo vya kutolea huduma na kutoka kituo kimoja kwenda kingine.

Pia, Dkt. Samizi amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa kuzingatia miongozo na ushahidi wa kisayansi, kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, kuimarisha huduma wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, pamoja na kuongeza uhamasishaji kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuanza kliniki mapema na kupata huduma stahiki.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *