Wananchi wahimizwa kuepuka mikopo umiza na itolewayo ta taasisi bubu

Na. Hafidhi Ally, Iringa

Wananchi wa Kata ya Boma, Halmashauri ya Mji Mafinga, wametakiwa kujiepusha na mikopo inayotolewa na taasisi zisizosajiliwa, ikielezwa kuwa imekuwa chanzo cha migogoro ya kifamilia na kuvuruga ndoa.

Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Boma, Baraka Kisakanike, wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevele Villa.

Kisakanike amesema baadhi ya taasisi zinazotoa mikopo hiyo zimekuwa zikiwafuatilia wadaiwa hadi majumbani kwao, wakati mwingine nyakati za usiku, jambo ambalo amesema limekuwa likisababisha taharuki na migogoro katika familia.

Amesema hali hiyo imefikia hatua ya baadhi ya wanawake wanaodaiwa mikopo hiyo kukimbia na kuziacha ndoa zao kutokana na shinikizo linalotokana na wadai.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevele Villa, amesema Serikali imeweka mifumo ya kuwawezesha wananchi kupata mikopo yenye masharti nafuu, ikiwamo mikopo yenye riba ya asilimia 10, kwa lengo la kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Aidha, amezitaka benki kuweka masharti rafiki kwa wananchi, akisema riba ya asilimia 18 inayotozwa kwenye baadhi ya mikopo inaweza kuwa mzigo kwa wakopaji na kusababisha kushindwa kurejesha madeni yao kwa wakati.

Katika ziata hiyo wananchi waliwasilisha kero zao ikiwemo changamoto ya barabara na maji ambapo Mbunge Villa amesema kuwa serikali itaendelea kutatua changamoto zote mara baada ya Bajeti kufika.

About The Author

Also Read  IFAD na TZ Wajadili uendelezaji wa Kilimo Biashara

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *