Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mhe. Dkt. Linda Selekwa, amewataka viongozi na wataalamu kuhakikisha wanatoa huduma kwa weledi, uadilifu na heshima kwa Watumishi na Wastaafu wanaofika kuwasilisha kero zao.
Mhe. Selekwa ametoa kauli hiyo wakati wa Kliniki ya kushughulikia kero za Watumishi na Wastaafu iliyofanyika katika Viwanja vya Halmashauri ya Mji Mafinga.
Amesema Serikali inatambua kuwa bado kuna changamoto zinazowakabili Watumishi na Wastaafu, hivyo imeweka utaratibu wa kuwasikiliza moja kwa moja ili kurahisisha utatuzi wa kero zao.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi Mkuu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Nuru Sovela, amewapongeza Watumishi kutoka Wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji Mafinga kwa kujitokeza na kuwasilisha changamoto zao.
Bi. Sovela amesema ushiriki huo utasaidia kuboresha ustawi wa Watumishi na kuongeza ufanisi katika utendaji wa Serikali.

Naye Mkuu wa Idara ya Utumishi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Ndugu Charles Mwaitege, amesema kliniki hiyo ni muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kikazi na kujenga mazingira bora ya utendaji kwa Watumishi.
Kliniki hiyo imefanyika ikiwa na kauli mbiu “Watumishi Iringa! Sema na Mwajiri,” ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha Watumishi na Wastaafu wanapata nafasi ya kuwasilisha kero zao, kusikilizwa na kupata huduma stahiki.






