Na. Gerwin Ntampera, Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Kampeni ya Okoa Mvuvi, unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, 2026 katika eneo la Uroa Pongwe, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kapt. Hamad Bakar Hamad, amesema kampeni hiyo imelenga kuimarisha usalama wa wavuvi na kuhakikisha wanaokolewa kwa haraka wanapokumbwa na majanga baharini.
Kapt. Hamad amesema kampeni hiyo inalenga kuwarasimisha wavuvi ili watambuliwe na kupata huduma za uokozi wanapokumbwa na matatizo wanapokuwa katika shughuli zao.
Amesisitiza kuwa uamuzi huo umetokana na takwimu zinazoonesha kuwa zaidi ya wavuvi 100 kwa mwaka hukumbwa na matukio ya kuzama ambapo asilimia 27 wakipoteza maisha pamoja na mali zao.
Ameongeza kuwa Wizara hiyo kwa kipindi cha miaka tisa imefanya utafiti kubaini maeneo mbalimbali ya uvuvi ambayo wavuvi wa Zanzibar hupendelea kwenda kuvua ambapo samaki hupatikana kwa wingi.
“Utafiti huo tumeshirikiana na Taasisi ya WorldFish kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Baharini (ZAFIRI) ili kubaini maeneo hayo na kuwalinda wavuvi,” amesema Cap. Hamad.
Amefafanua kuwa Wizara imechagua boti 100 ambazo zimefungwa vifaa maalumu vya kutoa ishara kupitia mfumo maalumu kwa mamlaka husika hatua inayolenga kurahisisha ufuatiliaji na uokozi wa wavuvi wanapokuwa baharini.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, taarifa zitakazopatikana kupitia mfumo huo zitagawanywa kwa vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo KMKM, ZMA na Shirika la Bandari, ili kusaidia kufahamu maeneo ambayo wavuvi huenda kuvua katika vipindi vya upepo mkali.






