Kata ya Boma Mafinga yapelekewa huduma ya maji ya visima

Na. Hafidhi Ally, RUJAT Iringa

Shirika la People Development Forum (PDF), kwa kushirikiana na Serikali, limeanza kutekeleza mradi wa uchimbaji wa kisima cha maji katika Mtaa wa Ihongole, uliopo Kata ya Boma, Halmashauri ya Mji Mafinga.

Akizungumza mara baada ya kuanza kwa uchimbaji wa kisima hicho katika Shule ya Msingi Mwongozo, iliyopo Mtaa wa Ihongole, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Festo Atanas Madenge, amesema mradi huo utasaidia wananchi wanaozunguka shule hiyo kupata huduma ya maji safi na salama.

Aidha, amewataka wananchi wa mtaa huo kujiandaa kuunganishiwa huduma ya maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MAUWASA), kwani kutakuwa na vituo vitakavyowezesha usambazaji wa maji hadi majumbani.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Ihongole wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo, wakisema utawasaidia kupata huduma ya maji ambayo wamekuwa wakiikosa kwa muda mrefu.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwongozo Atu Mung’ong’o amelishukuru Shirika la PDF kwa kuwapatia huduma hiyo ya maji, sambamba na kujenga vyoo 40 vya mashimo, hatua ambayo amesema itasaidia kuimarisha afya na ustawi wa wanafunzi shuleni hapo.

Mafundi wakiandaa mabomba kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa uchumbaji wa visima vya maji na usambazaji kwa wananchi

Nao wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwongozo wameishukuru Serikali kwa kuwakaribishia huduma ya maji ya kisima, wakisema awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji, hali ambayo ilikuwa ikiathiri masomo yao.

About The Author

Also Read  TRA Kigoma yatangaza neema kwa Wafanyabiashara Wadogo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *