Wafanyabiashara Mafinga washauriwa kushirikiana na serikali kimkakati

Wafanyabiashara wa Soko Kuu Mafinga wameshauriwa kukaa pamoja na Serikali katika mashauriano, ili kufikia mwafaka kuhusu ujenzi wa soko hilo kupitia Mradi wa TACTIC unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, wakati akizungumza na wafanyabiashara hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika wakati wa ziara yake ya kikazi.

Mbunge Villa amesema utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa Soko Kuu, Stendi ya Mabasi pamoja na barabara za lami, hatua inayolenga kuboresha miundombinu na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Manispaa ya Mafinga.

Aidha, Mbunge Villa ameitaka Serikali kuhakikisha wafanyabiashara watakaohamishwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo wanapelekwa katika maeneo yanayofaa kwa ajili ya kuendelea na shughuli zao za biashara.

Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wakisikiliza kwa kina maelezo kuhusu miradi ya TACTIC

Kwa upande wake, Mratibu wa TACTIC katika Halmashauri ya Mji Mafinga, Joseph Temba, amewataka wafanyabiashara kuondoa hofu, akisisitiza kuwa utekelezaji wa mradi utazingatia kanuni, taratibu na sheria. Amesema wafanyabiashara watashirikishwa katika kila hatua ya mchakato.

Awali, Katibu wa Soko Kuu Mafinga, Victor Mgani, maarufu kama Mr. Bookshop, akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, aliiomba Serikali kupitia Mbunge kuwapa muda wa kukaa kwenye mazungumzo na Serikali ili kufikia makubaliano, badala ya kuwahamisha bila majadiliano.

Mradi wa TACTIC, unaotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, unalenga kuboresha miundombinu katika Halmashauri ya Mji Mafinga, ikiwemo ujenzi wa Soko Kuu, Stendi ya Mabasi na barabara za lami, kwa lengo la kukuza shughuli za kiuchumi na kuboresha huduma za kijamii.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *