Na. Neema Mtuka, Sumbawanga
Rukwa: Wakati Mkoa wa Rukwa ukiadhimisha Siku ya Afya ya Mazingira Duniani Septemba 26, wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga wameibua kilio cha kukosekana kwa madumu ya kuhifadhia taka (dustbin) katika maeneo ya hadhara, hali inayochangia utupaji wa taka hovyo.
Wananchi hao wametoa ombi hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
“Tunaomba Serikali ituwekee vitunza taka kila mahali, sokoni, stendi na barabarani. Ukitembea na chupa ya maji unakosa pa kuitupa, mwisho unaona aibu na unaitupa chini. Tukipata vitunza taka tutaweza kutunza mji wetu uwe safi,” amesema Rehema Juma, mfanyabiashara wa Soko la Mandela.
Mfanyabiashara Juma Said, amesema kuwa serikali inapaswa kuwaelimisha wananchi juu ya usafi wa mazingira na utunzaji wa taka.
“Tumeelimishwa kutotupa taka hovyo, lakini miundombinu ya kutupa taka yenyewe haipo. Halmashauri itusaidie.” Amesema Said
Akijibu kilio hicho, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,Charles Makongoro Nyerere, amesema serikali imesikia ombi hilo na kuitaka halmashauri kulifanyia kazi mara moja.
“Nimeyasikia malalamiko yenu kuhusu dustbin, ni ombi la msingi sana. Afya ya mazingira inaanzia na uwepo wa miundombinu ya kutunza taka. Namuagiza Mkurugenzi wa Manispaa kuhakikisha vitunza taka vinawekwa katika maeneo yote ya mikusanyiko. Lakini wananchi pia muwe walinzi wa vifaa hivyo msiviharibu,” amesema RC Nyerere.
Ameongeza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yake yanakuwa safi ili kujikinga na magonjwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile, amesema licha ya changamoto ya uchafu, wilaya itaendelea kusimamia sheria za afya.
“Uchafu ndio chanzo cha magonjwa mengi kama kipindupindu. Tutaendelea kutoa elimu na kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka sheria za usafi.
“Usafi si wa siku moja ya maadhimisho, ni tabia ya kila siku,” amesema Chirukile.
Naye Afisa Afya wa Mkoa wa Rukwa, Martin Emanuel, amesema kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza jamii kutambua mazingira safi ni haki na wajibu wa kila mtu ambayo ni nguzo muhimu katika kulinda afya ya jamii.
“Jukumu letu kama wataalamu wa afya ni kuendelea kutoa elimu juu ya utenganishaji wa taka na matumizi sahihi ya vyoo bora ili kupunguza magonjwa yatokanayo na mazingira machafu,” alisema Emanuel.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa zoezi la usafi katika Soko la saba Saba lililopo mjini Sumbawanga.






