Kigoma yatangaza kufanyika kwa Tamasha kubwa la kabila la Waha mwaka huu

Na. Mwandishi wetu, Kigoma

Wananchi Mkoani Kigoma na Waha wanaoishi sehemu mbalimbali nchini Tanzani ana duniani kwa ujumla, wamepewa wito wa kujitokeza kuunga mkono na kushiriki tamasha la Buha 2026 lililotangazwa rasmi na jamii ya Waha kama jukwaa linalolenga kujenga mahusiano, ushirikiano na maendeleo ya jamii na kuenzi urithi wa Buha.

Akizungumza na wandishi wa habari Mkoani kigoma Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha la Buha 2026 Stewart Ernest Zindutse amesema urithi wa buha ni sehemu ya utajiri katika utamaduni wa Tanzania hivyo tamashaa hilo linakusudiwa  kuwa jukwaa la kutangaza  lugha, historia, mila na desturi kuendelea kurithishwa kizazi hadi kizazi.

Zindutse amesema tamasha hilo linatoa fursa kwa wajasiriamali, vikundi vya wanawake na vijana, wasanii na wafanyabiashara kuonyesha bidhaa na kazi zao.

TAMASHA la utamaduni wa kabila la Waha mkoa Kigoma linaelezwa litatumika kutangaza fursa na vivutio mbalimbali vya uwekezaji mkoani Kigoma ikiwemo kwenye masuala ya utalii na malikale.

Mwenyekiti wa Kamati ya Tamasha la Buha 2026 Kasulu, akitzungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma, Kulia ni Dkt. Peter Mayengo anayefanya kazi nchini Sudan Kusini ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo, na wa mwisho (kulia) ni Aron Chishako mfanya biashara na mjumbe wa kamati

Mwenyekiti huyo alisema kuwa tamasha hilo limeungwa mkono na wananchi wenye asili ya mkoa Kigoma wanaoishi nchi mbalimbali duniani ambapo wamekubali kushiriki tamasha hilo na kubeba ajenda ya kutangaza utamaduni wa kabila la Waha Kimataifa

Alisisitiza kuwa Tamasha hili limeandaliwa na umoja wa Ibhuha Yachu likiwa na lengo la kuwakutanuisha waha wanaoishi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi ili kuenzi urithi wa buha na  kujadili mshikamano katika kuchangia maendeleo ya mkoa wa kigoma.

Also Read  Wananchi Kalenga-Iringa wakerwa na uchakavu wa barabara, Mbunge atoa hoja

Naye Dkt. Peter Mayengo ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo amesema licha ya kutangaza na kuenzi urithi wa tamaduni za buha vijana watakuwa na nafasi ya kujifunza fursa zinazopatikana katika matumizi ya teknolojia kujiongezea kipato

Aidha Mwenyekiti kamati ya habari na mawasiliano wa umoja wa Buha Yetu Prosper Kwigize amesema pamoja na maonesho mbalimbali, pia wanakigoma watapata fursa ya elimu ya uraia na uzalendo katika tamasha hilo.

Ndg. Prosper Kwigize (kulia) Mwenyekiti wa kamati ya Habari na mawasiliano ya maandalizi ya Tamasha la Buha 2026 akifafanua jambo kuhusu Tamasha hilo.

Kwigize alisema kuwa pamoja na kuonyesha mavazi, vyakula na mambo mbalimbali yenye aasili ya kabila la Waha lakini pia watatumia nafasi hiyo kuibua ajenda ya kuhifadhi utamduni wa Kabila la Waha katika teknolojia ya sasa ya mawasiliano ya kidijitali sambamba na kutumia akili mnemba (AI) kutangaza fursa Chanya za ukanda wa magharibi mwa Tanzania.

Aliongeza kuwa awali kabla na wakati wa Ukoloni wa Ujerumani, Ubelgiji na Uingereza Kigoma ilikuwa inajulikana kama Buha kutokana na Kabila la Waha lakini baada ya mabadiliko ya tawala mbalimbali hilo lilibadilika na mkoa huo kuitwa Kigoma hivyo asili ya Buha inapotea hivyo tamasha hilo litaeleza historia hiyo kwa jamii kubwa ya Watanzania ndani na nje ya nchi.

Tamasha la Buha 2026 linatarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 17-19 2026 katika uwanja wa Michezo wa UMOJA mjini Kasulu likiwa na kaulimbiu ya “Tukumbuke asili, Tujenge Umoja na Maendeleo” hivyo waha wanaoiishi Tanzania na nje ya Tanzania, wasanii, wanazuoni, taasisi binafsi na za umma hawana budi kushiriki.

Also Read  Londo ashuhudia kipaji cha watoto wakiielezea WMA

Zaidi ya washiriki 5000 wakiwemo Waha wanaoishi na kufanya kazi katika mataifa ya Ulaya, Asia na Marekani, taasisi za michezo, taasisi za fedha, Utalii, kilimo na biashara watahudhuria tamasha hilo ambali litakuwa la kwanza kufanyika mkoani Kigoma. Awali matamasha kadhaa yalifanyika katika Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam

Miongoni mwa vivutio vya Kabila la Waha ni pamoja na historia za kichifu hususani Mwami Theresia Ntare Mwanamke pekee aliyeongoza Waha upande wa Heru Juu, wengine ni Mwangi Ruhaga, Nyamaliza, Bharegenyeza, Ruhinda, Kimenyi na wengine.

Aidha vivutio vingine ni mavazi ya asili yatokananyo na magome ya miti, vyakula asilia, ngoma na nyimbo za utamaduni.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *