Na Angela Sebastian, RUJAT Kagera
Mahakama ya Wilaya ya Karagwe imemtia hatiani Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chagati, Robson Andrea Nganshinga, kufungwa jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi 500,000 baada ya kupatikana na hatia ya kosa la rushwa lililohusisha utoaji wa barua ya utambulisho kwa mtu aliyedaiwa kuwa si raia wa Tanzania.
Hukumu hiyo imetolewa na na Hakimu Mkazi Mwandamizi (SRM), Charles Ngonyani, katika shauri la rushwa namba 15343/2026.
Akizungumza leo, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kagera, Ismail Bukuku, amesema mshtakiwa alishtakiwa kwa kosa la rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(b) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA), Sura ya 329.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Nganshinga aliidhinisha barua iliyomtambua Fabuan John, anayejulikana pia kama Dusabimana Fabiice, kuwa ni mkazi na raia wa Tanzania ili aweze kupata ajira katika Kiwanda cha Kukoboa Kahawa (KDCU), huku akijua kuwa mtu huyo alikuwa raia wa Burundi.
Baada ya kusikiliza ushahidi uliowasilishwa mahakamani, mahakama ilimkuta mshtakiwa na hatia na kumhukumu kulipa faini ya shilingi 500,000 au kufungwa miaka mitatu jela amnapo mshtakiwa alilipa faini hiyo.
Shauri hilo liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Mohamed Kassim Mtambo,
hatua hiyo inaendelea kuonyesha msimamo wa mamlaka za kupambana na rushwa katika kuwawajibisha watumishi na viongozi wanaobainika kukiuka sheria, hususan katika masuala yanayohusu utoaji wa nyaraka za utambulisho na huduma za umma.






