TanzanEye yafadhili kituo cha tiba ya macho, wagonjwa milioni 2 kutibiwa kila mwaka Kigoma

Na. Gerwin Ntampera, Kigoma

Katika kuadhimisha Siku ya Macho Duniani, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Yosefu Kabanga, wilayani Kasulu mkoani Kigoma, imezindua jengo jipya la wagonjwa wa nje, upasuaji na huduma za kibingwa za macho,

Uzinduzi huo umefanywa na RAIS wa Mabaraza ya Maaskofu ya Kanisa Katoliki kwa Nchi za Ukanda wa Mashariki mwa Africa (AMECEA) ambaye pia Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Mhashamu Gerevas Nyaisonga, akishirikiana na Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Mhashamu Joseph Mlola.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhashamu Gerevas Nyaisonga (mgeni rasmi) amesema huduma za macho ni sehemu muhimu ya afya ya mwanadamu, kwa kuwa uwezo wa kuona humwezesha mtu kufanya shughuli za kila siku kwa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya familia na taifa. Amesisitiza pia umuhimu wa kuwahudumia wagonjwa kwa utu na heshima.

RAIS wa Mabaraza ya Maaskofu ya Kanisa Katoliki kwa Nchi za Ukanda wa Mashariki mwa Africa (AMECEA) Mhashamu askofu Gerevas Nyaisonga

Kwa upande wake, Luteni Kanali Joseph Kadala Mrimi aliye mwakilisha mkuu wa mkoa wa Kigoma Balozi Simoni Sirro amesema Serikali inapongeza Kanisa Katoliki na wadau wa maendeleo kwa uwekezaji huo, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na wadau ni muhimu katika kuboresha huduma za afya.

Amesema jengo hilo linapaswa kwenda sambamba na wataalamu, vifaa tibana matibabu bora na amewataka wananchi kuweka afya ya macho katika vipaumbele vyao kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara na kufuata ushauri wa wataalamu.

Mkuu wa wilaya ya Kasulu Luten Kanali Joseph Kadala Mrimi aliye mwakilisha mkuu wa mkoa wa Kigoma Balozi Simoni Sirro

Aidha, mkuu wa mkoa wa Kigoma amewatahadharisha wananchi dhidi ya tabia ya kutumia dawa za macho bila ushauri wa wataalamu, akisema matumizi holela ya dawa yanaweza kusababisha madhara na hata kupoteza uwezo wa kuona.

Also Read  MO awapa somo la maisha wanachuo RUCU, kutumia fursa za kiuchumi

Dkt. Kasten Paust, mwanzilishi na mkurugenzi mkuu wa TanZanEye, amesema mradi huo ni zaidi ya mpango wa afya, ni ishara ya ushirikiano na urafiki kati ya Tanzania na Ulaya akisisitiza kuwa jengo hilo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za macho Kigoma, huku akiweka bayana kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha huduma hizo zinakuwa bora na endelevu.

Dkt. Kasten Paust, mwanzilishi na mkurugenzi mkuu wa TanZanEye

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kabanga, Dkt. Peter James Kitenge, amesema hospitali hiyo inahudumia zaidi ya watu milioni 2.3 kwa mwaka.

Kupitia kambi nane za matibabu ya macho, zaidi ya watu 3,692 wamepatiwa huduma, wakiwemo 993 waliofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, huku watumishi 38 wakipatiwa mafunzo katika fani mbalimbali za macho.

Mradi huo umefadhiliwa na TanZanEye kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 1.057, ikijumuisha ujenzi, samani na vifaa tiba.

Huduma hizo zinatarajiwa kuwanufaisha wananchi wa Kigoma pamoja na mikoa jirani ya Katavi, Rukwa na Kagera, huku hatua inayofuata ikiwa ni kukamilisha baadhi ya miundombinu na kuongeza vifaa vya kibingwa ili huduma bora za macho ziendelee kupatikana kwa wananchi sasa na vizazi vijavyo.

Picha ya Pamoja ya viongozi baada ya kuzindua jengo la tiba ya macho katika hospitali ya rufaa Kabanda, Kutoka kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kasulu Luteni Kanali Mrimi, Mhashamu Askofu Nyaisonga, Mhashamu askofu Mlola na mkurugenzi wa TanzanEye Bw. Kasten

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *