Na. Mwandishi wetu, Kigoma
Uongozi bora na usimamizi madhubuti wa rasilimali za vyama vya ushirika umetajwa kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya ushirika, huku viongozi wakihimizwa kufanya maamuzi yanayozingatia sheria, uwajibikaji, pamoja na kulinda maslahi na haki za wanachama wote.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaack Mwakisu amesema hayo leo Juni 29,2026 wilayani humo wakati akifungua Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika la Mkoa wa Kigoma lililowakutanisha washiriki kutoka vyama mbalimbali vya ushirika vinavyotoka katika halmashauri zote nane za mkoa huo.
Aidha, Kanali Mwakisu ametaka vyama vya ushirika vihakikishe vinakua na kumiliki biashara kubwa, ikiwa ni pamoja na kupanua shughuli zake hadi kufikia hatua ya kuwa na kipato kinachotokana na uwekezaji wao wenyewe.
“Mkoa wa Kigoma una fursa nyingi zikiwemo kilimo,utalii na biashara za mipakani…zitumieni fursa hizo ili ushirika mnaoufanya uwe ni ule unaojitegemea pasipo kusubiria fedha za nje na mkifikia hatua hiyo inakuwa rahisi kwenu kukopesheka,” amesema.

Naye Mrajisi Msaidizi Mkoa wa Kigoma, Richard Majalla amesema kuwa jukwaa hilo la siku mbili litawapa washiriki fursa ya kufanya tathmini ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja, pamoja na kubaini changamoto zilizojitokeza ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu, Nelson Swai amesema kuwa endapo katika utekelezaji wa majukumu ya msingi mtu atajipatia manufaa binafsi kupitia mnyororo wa utoaji huduma katika vyama vya ushirika, atakuwa ametenda kosa chini ya kifungu cha 23 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Jukwaa hilo linatarajiwa kufikia tamati kesho likiongozwa na kauli mbiu isemayo “Ushirika kwa Ulimwengu Wenye Amani” Linda Ushirika, Chagua Uadilifu na litafungwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Sirro.






