Polisi Mkoani Iringa yawacharukia makampuni binafsi ya Ulinzi

Na. Hafidhi Ally – RUJAT Iringa

Jeshi la Polisi mkoani Iringa limetangaza kiama kwa kampuni za ulinzi ambazo zimekuwa zikikiuka sheria na kanuni za vibali vya ulinzi, hali inayodaiwa kusababisha malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, SACP Allan Bukumbi amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wamiliki wa kampuni za ulinzi kuajiri watu wasio na vigezo sambamba na kuwapa silaha bila kuwapatia mafunzo stahiki sambamba na kuwacheleweshea mishahara wafanyakazi wao.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Kampuni Binafsi za Ulinzi Tanzania (TISIA) Mkoa wa Iringa, Alexander Mkumbo amekiri kuwa ukosefu wa mshikamano na ushirikiano miongoni mwa kampuni binafsi za ulinzi umekuwa chanzo cha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo mkoani Iringa.

Nao Polisi Kata Jamii Wilaya ya Iringa wamesema kuwa licha ya kufanya kazi kwa karibu na Kampuni Binafsi za ulinzi bado kumekuwa na changamoto za kutoheshimiwa na watendaji wa Kampuni hizo.

Makamanda wa Jeshi la polisi mkoani Iringa katika Picha ya pamoja na viongozi wawakilishi wa makampuni binafasi ya Ulinzi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limeeleza kuwa hatua hizo zinalenga kuhakikisha sekta ya ulinzi binafsi inafanya kazi kwa kuzingatia sheria, taaluma na usalama wa wananchi.

Makampuni binafsi ya ulinzi yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika ulinzi wa watu na mali zao kazi ambayo hutekelezwa na jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.

Baadhi ya makampuni binafsi ya ulinzi humilikiwa na vikundi vya wana taaluma za ulinzi kama vile SUMA JKT, na Muungano wa Wanajeshi Wastaafu Tanzania MUWAWATA

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *