Na. Fadhili Abdallah, RUJAT Kigoma
WAZAZI na vijana wanatarajia kuletwa pamoja kuzungumzia changamoto zinazosababisha kuporomoka kwa maadili katika eneo la Ujiji ikiwa ni sehemu ya Tamasha la Historia na utamaduni wa mji wa Ujiji limalotarajia kufanyika kwa siku mbili kuanzia juni 21 mwaka huu.
Mkuu wa Historian na Mali kale wa Taasisi ya Ujiji Heritage and Developoment Hamisi Hababi alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari akieleza kufanyika kwa tamasha hilo na kubainisha kwamba Ujiji imekumbwa na changamoto kubwa ya kuporomoka kwa maadili hivyo kuacha mila na tamaduni za maisha ya watu wa Ujiji kuachwa.
Tamasha hilo pamoja na mambo mengine litakuwa na maonyesho ya mambo mbalimbali ya asili ya Ujiji ikiwemo vyakula na mavazi ambapo pia mikutano na makongamano yatafanyika kuzungia maendeleo ya mila na tamaduni za eneo hilo sambamba na changamoto zinazojitokeza na kufanya mila hizo na desturi kuachwa.

Aidha Kiongozi huyo alisema kuwa Tamasha hilo litatumika pia kuhamaisha shughuli za utalii zinazofanyika mkoani Kigoma katika vivutio vya utalii ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Gombe maarufu kwa uhifadhi wa Sokwe, kituo cha Livingistone maarufu kwa historia ya mambo ya utumwa, maisha ya wananchi na tamaduni za kale za wananchi hao.
Akizungumza katika mkutano huo Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Taasisi hiyo, Iddi Rajabu Mvano alisema kuwa katika tamasha hilo pia wamealika watu mbalimbali maarufu akiwemo Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Star, Sunday Manara.
Mvano alisema kuwa wakati wa tamasha hilo michezo mbalimbali na mbio fupi zitafanyika, ngoma za asili za makabila ya Ujiji na kutembelea maeneo mbalimbali waliokuwa wakiishi watu mbalimbali waanzilishi wa mji wa Ujiji, majengo ya kale, visima vya maji na namna ya maisha ya jumla ya watu hao.






