Jeshi la Zima moto na uokoaji latoa mafunzo kwa vijana mkoani Iringa

Na. Hafidhi Ally – RUJAT Iringa

Zaidi ya vijana 200 kutoka vijiji 61 vinavyozunguka Shamba la Miti la Taifa la Sao Hill, Wilaya ya Mufindi, wamepata mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uhifadhi wa misitu na mazingira.

Akizungumza wakati wa usaili wa vijana zaidi ya 400 waliojitokeza kupima utimamu wa mwili na akili, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti la Sao Hill, PCO Said Singano, amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za kuhakikisha wananchi wanaozunguka shamba hilo wanashiriki kikamilifu katika kulinda misitu dhidi ya majanga ya moto.

Afisa wa vikosi vya Jeshi la Zimamoto akiwaandaa vijana tayari kupata mafunzo maalumu ya zima moto na uakoaji

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo vijana katika mbinu za kuzuia, kudhibiti na kukabiliana na moto wa misitu, pamoja na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kulinda rasilimali za taifa.

Vijana waliojitokeza kupata mafunzo hayo wamesema kuwa hatua hiyo itasaidia kukabiliana na majanga ya moto kwani misitu imekuwa na faidha katika maisha ya binaadamu.

Kwa upande wake, Afisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Mufindi, Sajenti Guntramu Mlenge, amesema ushirikiano kati ya jeshi hilo na Sao Hill umeendelea kuzaa matunda kupitia utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti Sao Hill imekuwa na utaratibu wa kukabiliana na majanga ya moto wa misitu kwa kuendesha usaili wa watumishi wa muda watakaounda vikosi maalumu vya kuzuia, kudhibiti na kuzima moto katika maeneo ya shamba na maeneo yanayolizunguka.

Also Read  MO awapa somo la maisha wanachuo RUCU, kutumia fursa za kiuchumi

 

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *