Mbunge Ngajilo hapoi, akemea wazazi kuficha watoto

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Fabiani Ngajilo, amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu majumbani, akisisitiza kuwa watoto hao wana haki ya kupata elimu sawa na watoto wengine na wanapaswa kupewa fursa ya kutimiza ndoto zao.

Ngajilo ametoa wito huo wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya shule na msaada wa chakula kwa watoto wanaotoka katika familia zenye uhitaji, iliyofanyika katika Shule ya Msingi Ugele, Kata ya Mkimbizi, Manispaa ya Iringa.

Amesisitiza kuwa watoto wenye ulemavu hawapaswi kufichwa wala kunyimwa haki zao za msingi, bali wanapaswa kuandikishwa shule na kupewa fursa sawa ya kupata elimu, kwani wana uwezo wa kufaulu na kuchangia maendeleo ya jamii kama watoto wengine.

Akizungumza na wananchi, Ngajilo amesema msaada huo unalenga kupunguza changamoto zinazowakabili watoto wanaotoka katika familia zenye uhitaji ili waweze kuhudhuria masomo bila vikwazo vinavyotokana na ukosefu wa mahitaji muhimu.

Baadhi ya wazazi na walimu waliohudhuria hafla hiyo walieleza kuwa msaada huo utasaidia kupunguza mzigo kwa familia zenye uhitaji na kuwawezesha watoto wengi kuendelea na masomo bila kukabiliwa na upungufu wa vifaa muhimu vya kujifunzia.

Katika hafla hiyo, watoto walikabidhiwa vifaa mbalimbali vya shule pamoja na vyakula vikiwemo mahindi, maharage na mafuta ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwasaidia kupata mazingira bora ya kujifunzia.

About The Author

Also Read  Wakala wa Vipimo wavutia wageni maonesho ya Nane Nane

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *