Imeelezwa kuwa jamii inaweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kufuatilia na kutumia taarifa rasmi za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika shughuli zake za kila siku.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 17, 2026 wilayani Kasulu na Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Wilaya, Hassan Lucas, wakati akifungua kikao cha utambulisho wa Mradi wa Green Alert unaotekelezwa na Taasisi ya Tanzania Wote Equality Alliance (TAWEA) kwa ufadhili wa CAF America.
Lucas amewahimiza wananchi kutumia taarifa za TMA kupanga shughuli zao za kila siku ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na changamoto hizo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi kutoka TAWEA, Festo Mrina, amesema mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili katika kata tano za Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na unatarajiwa kuwafikia zaidi ya wananchi 30,000.
Amesema elimu itatolewa kupitia mikutano ya hadhara, vipindi vya redio, mitandao ya kijamii na jumbe fupi za sauti zilizorekodiwa, ili wananchi wapate taarifa sahihi zitakazowawezesha kupanga shughuli zao kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Naye Meneja wa Hali ya Hewa Mkoa wa Kigoma, Mugisha Kyaruzi, amesema ushiriki wa TMA katika mradi huo utasaidia kuifikishia jamii taarifa sahihi za hali ya hewa na kupunguza utegemezi wa taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
Mradi wa Green Alert ulianza Aprili 2026 na unatarajiwa kukamilika Machi 2028 ambapo utatekelezwa katika kata za Nyamidaho, Kurugongo, Makere, Kitagata na Kabulanzwili.






