Wananchi wa Kata ya Ulanda, Jimbo la Kalenga, wameeleza malalamiko yao kuhusu gharama kubwa ya vibali vya ujenzi, wakidai kuwa inawazuia kujenga nyumba za kisasa.
Wakizungumza na Nuru FM baada ya mkutano wa hadhara wa Mbunge, wananchi wa vijiji vya Mwambao na Weru wamesema kuwa, pamoja na kuhamasishwa kujenga nyumba bora, wanalazimika kulipa shilingi elfu 50 ili kupata kibali cha ujenzi, kiwango ambacho wengi wanakiona kuwa ni kikubwa.
Aidha, wananchi hao wamedai kuwa gharama hiyo pia hutozwa hata pale wanapofanya ukarabati wa nyumba za zamani za tope kwa lengo la kuziboresha na kuzifanya za kisasa.
Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amesema kuwa Baraza la Halmashauri lina mamlaka ya kutunga sheria ndogondogo zinazolenga kuongeza vyanzo vya mapato kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo katika halmashauri.
Hata hivyo, Kiswaga amesema atafanya mazungumzo na Halmashauri ili kutafuta namna ya kupunguza gharama ya kibali cha ujenzi, akieleza kuwa kiwango cha sasa kinaonekana kuwa kikubwa kwa wananchi wenye vipato vya chini.






