Nane Nane yachochea matumizi ya teknolojia na ubunifu kanda ya Magharibi

Na. Mwandishi wetu, Tabora

Maonesho ya Nanenane yameelezwa kuwa jukwaa muhimu katika kuchochea mabadiliko katika sekta ya uzalishaji kupitia teknolojia, elimu na ubunifu unaowafikia wakulima, wafugaji na wadau mbalimbali wa kilimo katika maeneo yao.

Hayo yameelezwa leo, Agosti 8, 2026, na Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Mhe. Dkt. Jafari Rajabu Seif, wakati akifunga Maonesho ya Nanenane kwa Kanda ya Magharibi yaliyofanyika katika Viwanja vya Ipuli mkoani Tabora.

Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Mhe. Dkt. Jafari Rajabu Seif

Mhe. Seif amesema maonesho hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea ushirikiano wa karibu kati ya wakulima, wafugaji, wajasiriamali na taasisi za kifedha, jambo linalosaidia kukuza uzalishaji na uchumi wa nchi.

“Kimsingi, maonesho haya yanachochea ushirikiano wa karibu kati ya wakulima, wafugaji, wajasiriamali na taasisi za kifedha. Ndiyo maana yanafanyika kama sehemu ya kutambua mchango wao katika maendeleo endelevu na kukuza uchumi hapa nchini,” amesema.

Amesema pamoja na mafanikio yanayopatikana kupitia maonesho hayo, bado kuna umuhimu wa kuhakikisha elimu na teknolojia zinazooneshwa zinawafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo wanayoishi na kufanya shughuli za uzalishaji.

Baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro wakifuatana na Mgeni Rasmi

Kutokana na wananchi wengi kutofika katika ofisi za Serikali kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu kilimo, Mhe. Seif amewaelekeza maafisa ugani kuhakikisha teknolojia na mbinu mbalimbali zilizooneshwa katika maonesho hayo zinafikishwa hadi ngazi za kata na vijiji, ili kuwajengea wananchi uwezo wa kuzitumia katika kuongeza tija na uzalishaji.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Balozi Simon Sirro, amesema ameridhishwa na namna wajasiriamali walivyotekeleza agizo alilolitoa mwaka jana la kuhakikisha bidhaa zao zinawekwa katika vifungashio bora.

Also Read  Kimbembe cha Ubunge Isimani chaanza, Mtatifikolo apanda jukwaa

Amesema utekelezaji wa agizo hilo umeongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali hao na kuimarisha mnyororo wa thamani wa bidhaa zao, hatua inayosaidia kuongeza ushindani wa bidhaa katika soko.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *