Na, Egidia Vedasto, RUJAT, Arusha.
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imetangaza kutokubalika kwa maombi yaliyowasilishwa na raia wa Afrika Kusini, Patroklos Tsaperas, dhidi ya Serikali ya Malawi, baada ya kubaini kuwa hakukamilisha taratibu za ndani za kisheria na aliwasilisha maombi hayo nje ya muda unaofaa.
Uamuzi huo umetolewa leo Novemba 13, 2026, kufuatia shauri lililohusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika kesi zilizokuwa zinasikilizwa na mahakama za kitaifa nchini Malawi.
Tsaperas, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Malawi Mobile Limited (MML), aliishitaki Serikali ya Malawi akidai kuwa ilikiuka haki zake za kumiliki mali, kutobaguliwa, ulinzi sawa mbele ya sheria, kutambuliwa kama mtu mbele ya sheria na haki ya kusikilizwa kwa haki.
Katika maombi yake, alieleza kuwa ukiukwaji huo ulikiuka masharti ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), huku akiomba pia alipwe fidia.
Aidha, kabla ya kuanza kusikiliza hoja za msingi, Mahakama ilijiridhisha kuwa ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuzingatia kuwa Malawi ni mwanachama wa Itifaki ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo tangu Oktoba 9, 2008, na ilikuwa imewasilisha tamko linaloruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuwasilisha maombi moja kwa moja.
Mahakama pia ilibaini kuwa ilikuwa na mamlaka ya msingi, muda na kieneo kwa kuwa madai yalihusu haki zinazolindwa na mikataba ambayo Malawi ni mwanachama wake, baadhi ya matukio yalitokea baada ya nchi hiyo kujiunga na Itifaki na ukiukwaji uliodaiwa ulitokea ndani ya eneo lake.
Mahakama imeeleza kuwa katika kuchunguza uhalali wa maombi hayo, Serikali ya Malawi iliwasilisha mapingamizi mawili ikidai kuwa Tsaperas hakukamilisha taratibu za ndani za kutafuta haki na kwamba maombi yake yaliwasilishwa baada ya kupita muda unaofaa.
Kuhusu madai ya haki ya kumiliki mali, Mahakama ilibaini kuwa Tsaperas alikuwa ameonyesha uhusiano wa kutosha na kampuni ya MML kupitia umiliki wa hisa kwa njia isiyo ya moja kwa moja, huku kesi iliyofunguliwa na kampuni hiyo katika Mahakama Kuu ya Rufaa ya Malawi ikiwa imewasilisha kiini cha mzozo huo. Hivyo, ilikubaliana kuwa alikuwa amekamilisha taratibu za ndani kuhusu dai hilo.
Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa hakukamilisha taratibu hizo kuhusu madai mengine, ikiwemo kutokuwa na idadi ya kutosha ya majaji katika Mahakama Kuu ya Rufaa wakati wa kutoa hukumu, kutotekelezwa kwa hukumu ya kikatiba, ubaguzi kwa misingi ya utaifa na rangi pamoja na haki ya kutambuliwa kama mtu mbele ya sheria.

Katika pingamizi la pili, Mahakama ilibaini kuwa hukumu ya Mahakama Kuu ya Rufaa ya Malawi ilitolewa Machi 10, 2015, huku maombi dhidi ya Serikali hiyo yakiwasilishwa Oktoba 17, 2022, sawa na miaka saba, miezi saba na siku saba.
Mahakama imesema kipindi hicho kilikuwa kirefu kupita kiasi na hakukuwa na sababu za msingi zilizotolewa kueleza kuchelewa huko, hivyo maombi hayo hayakuwasilishwa ndani ya muda unaofaa.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilikubaliana na pingamizi la Serikali ya Malawi na kutangaza maombi hayo kuwa hayakubaliki bila kuendelea kuchunguza masharti mengine ya ukubalifu.
Pia iliamua kila upande kubeba gharama zake baada ya kubaini kuwa Serikali haikuthibitisha kuwa ilitumia gharama zozote katika shauri hilo.
Vile vile Jaji Suzanne Mengue aliambatisha maoni tofauti katika uamuzi huo kwa mujibu wa Itifaki ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo.






