Na Mwandishi wetu, Dodoma
Bodi ya usimamizi wa mfumo wa Stakabadhi za Ghala nchini Tanzania unaosimamiwa na wizara ya Viwanda na Biashara inasherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwake kwa kushuhudia mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake na kwa kuwaletea faidi wazazishaji na wafanya biashara wa mazao nchini
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, akiongea na waandishi wa habari amebainisha kuwa jumla ya kilo 1,122,246,475 za za mazao mbalimbali ambayo yamesajiliwa na Bodi kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala ikiwemo korosho, ufuta, kahawa, kakao, mbaazi, dengu, choroko, soya na chai ziliuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika minada ya kidijitali inayosimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Bw. Bangu ameweka bayana kuwa mauzo ya kilo bilioni 1.1 za mazao tisa yaliuzwa kupitia minada ya kidijitali katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku wakulima na wauzaji wakilipwa jumla ya Sh. trilioni 2.298 na kuchangia ongezeko la asilimia 43.6 la kiasi cha mazao yaliyouzwa kupitia mfumo huo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Bangu alisema kiasi hicho ni ongezeko la zaidi ya kilo milioni 340 ikilinganishwa na kilo 781,659,285 zilizokuwa zimeuzwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Ndani ya mwaka mmoja tumeshuhudia ongezeko kubwa la mazao yanayouzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Hii inaonesha wakulima wengi zaidi wanaendelea kuuamini mfumo rasmi wenye ushindani, uwazi na fursa bora za masoko,” alisema Bangu.

Imeelezwa kuwa wakati jamii ikiendelea kuwa na imani na mfumo wa stakabadhi za ghala kiwango cha pesa zinazowanufaisha wakulima moja kwa moja kimepanda ambapo zaidi ya Sh. trilioni 2.2 zilizolipwa kwa wakulima na wazalishaji, thamani ya biashara yote iliyofanyika kupitia mfumo huo ilifikia Sh. trilioni 2.679.
Bodi hiyo imebainisha kuwa, Serikali za Mitaa kupitia Halmashauri zilizosajili maghala zilikusanya Sh. bilioni 61.05 kupitia ushuru wa mazao, maarufu kama CESS, fedha zinazotarajiwa kuongeza uwezo wa Halmashauri kuboresha huduma za jamii na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Bangu alisema mafanikio hayo yamechangia kuongeza kipato cha wakulima na kuboresha ustawi wa kaya, huku fedha zilizopatikana zikiwezesha wananchi kugharamia mahitaji muhimu, yakiwemo elimu, afya na makazi, pamoja na kuwekeza katika shughuli za uzalishaji.
Alisema mapato ya CESS yameendelea kuwa nguzo muhimu kwa Halmashauri katika ujenzi na matengenezo ya barabara, shule, vituo vya afya, masoko na miundombinu mingine.
Katika hatua nyingine, akijibu swali la mwandishi wa habari kutoka RUJAT Bw. Prosper Kwigize kuhusu changamoto ya masoko ya mazao hususani Mahindi, maharage na Mhogo kutoka mikoa ya Magharibi yanayouzwa nchi jirani huku jamii ikikosa taarifa sahihi za masoko, Bw. Bangu ameahidi kufuatilia hali hiyo kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za wizara za kilimo, wizara ya viwanda na biashara ili kuwasaidi wananchi kupata masoko ya uhakika nje ya nchi kupitia mfumo mpya wa minada ya kidigitali
Aidha alitoa wito kwa wadau, wakulima na wafanya biashara wenye maghala kuendelea kuyasajili chini ya mfumo wa stakabadhi ya aghala ili kuwawezeha kupata bei na masokoo ya uhakika wa mazao, huku akibainisha kuwa kati ya takribani maghala 6000 ni maghala 446 pekee yaliyosajiliwa na bodi hiyo






