Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Paul John Wanga, amewataka wananchi kuwa na uelewa sahihi kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, akisisitiza kuwa asilimia hiyo siyo riba inayotozwa kwa wakopaji, bali ni jumla ya mgao wa fedha unaotengwa kwa makundi hayo kutoka katika mapato ya ndani ya Halmashauri.
Wanga amefafanua kuwa mikopo hiyo haitozwi riba yoyote, hivyo dhana kwamba mkopaji anapaswa kulipa asilimia 10 ya fedha alizokopa kama riba si sahihi na inaweza kupotosha umma kuhusu madhumuni ya mpango huo.
Akizungumza kuhusu mikopo hiyo kupitia Kikundi cha Maendeleo cha Wilaya ya Missenyi na mitandao ya kijamii, mwezi Novemba 2026, Wanga aliwataka wananchi, pamoja na wadau wanaofuatilia utekelezaji wa mpango huo, kuhakikisha wanapata na kusambaza taarifa sahihi ili mikopo hiyo iweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Alieleza kuwa jina la mikopo ya asilimia 10 linatokana na mgawanyo wa mapato ya ndani ya Halmashauri unaotengwa kwa makundi matatu ya wanufaika, ambapo wanawake hupangiwa 4% (yaani asilimia 40 ya mfuko) vijana 4% na watu wenye ulemavu 2%, na kufanya jumla ya 10%.
Kwa mantiki hiyo, alisema, asilimia 10 ni kiwango cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya makundi hayo na siyo gharama ya kukopa inayopaswa kulipwa na wanufaika.
Ufafanuzi huo unaungwa mkono na misingi ya kisheria inayosimamia utoaji wa mikopo hiyo nchini. Kanuni za Mikopo ya Halmashauri za mwaka 2019, Government Notice No.286, Kanuni ya 5(3), zinaeleza kuwa mikopo hiyo haitozwi riba.
Aidha, Kanuni mpya za mwaka 2024, Government Notice No.856, Kanuni ya 5(4), nazo zinasisitiza kuwa mikopo hiyo haitozwi riba, mfano, kundi linalopata mkopo wa shilingi milioni tatu,halitakiwi kurejesha fedha ya ziada kama riba ya asilimia 10. Linachopaswa kufanya ni kurejesha mkopo kwa mujibu wa masharti na utaratibu uliowekwa katika mpango huo.

Wanga alisisitiza kuwa lengo la Serikali kuanzisha mpango huo siyo kuwapatia wananchi fedha za kutumia bila mpango, bali kuwawezesha kupata mitaji ya kuanzisha biashara, kupanua shughuli za kiuchumi, kuongeza uzalishaji na kujiajiri.
Alieleza kuwa kurejeshwa kwa mikopo hiyo ni sehemu muhimu ya kuhakikisha fedha hizo zinaendelea kuzunguka na kuwafikia wanufaika wengine wenye mahitaji na mawazo ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Kwa mtazamo huo, urejeshaji wa mkopo haupaswi kutafsiriwa kuwa mkopaji hakunufaika na mpango huo, bali ni utaratibu unaowezesha mtaji uliotolewa kutumika na baadaye kuwafikia wengine.
Mpango huo una umuhimu mkubwa kwa vijana na makundi mengine yanayokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mitaji, hasa wale wenye mawazo na mipango ya biashara lakini wasiokuwa na uwezo wa kuanzisha shughuli hizo kutokana na ukosefu wa fedha.
Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, katika kipindi chake cha pili chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inalenga kuboresha maisha ya wananchi, wakiwemo wakazi wa Wilaya ya Missenyi, kupitia matumizi ya mapato ya ndani ya Halmashauri katika miradi na programu za kuwawezesha kiuchumi.
Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa mpango huo, kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masharti ya mikopo, utaratibu wa maombi, matumizi sahihi ya fedha na wajibu wa kurejesha mikopo kwa wakati.
Uelewa sahihi wa masharti hayo utasaidia kuondoa upotoshaji, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha mpango huo unatimiza lengo lake la kuwainua kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kwa ujumla, utoaji wa elimu kuhusu mikopo hiyo ni jambo la msingi, lakini elimu hiyo inapaswa kujengwa katika ukweli, takwimu na nyaraka rasmi za Serikali ili wananchi waweze kufanya maamuzi sahihi na kunufaika na fursa zilizopo.
Raphael Mwakibwala, Kaimu mkuu wa Divisheni ya maendekeo ya jamii katika Halmashauri ya Missenyi, amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/27, halmashauri hiyo imetenga sh bilioni 2.
Akitaja sifa za waombaji mikopo ni kwamba mtu awe na kitambukisho cha NIDA, kwa upande wa vijana, ni kuwa mtu awe na umri kuanzia miaka 18 hadi 45, na awe ndani ya kikundi cha watu watano.
Kwa wanawake ni umri wowote na awe ndani ya kukundi cha watu watano au zaidi, ilhali mwenye ulemavu anaweza kuomba peke yake, lakini kama wako zaidi kwenye eneo fulani wanaweza kuomba kama kikundi cha watu wawili au zaidi.
Ametaja mambo muhimu wanayotakiwa kuwa nayo waombaji kuwa ni barua za utambulisho toka mtendaji wa kijiji ,andiko la mradi, na taarifa za benki za kikundi husika.






