*MARIDHIANO NDIO SULUHU: DKT. SAMIA AMEFUNGUA MEZA, SASA TUIJAZE KWA HEKIMA*
Na. Dkt.Ahmad Sovu, Dar es Salaam
Jana, Jumatatu, Novemba 16, 2026, inaweza kuwa ni siku ya kukumbukwa katika historia ya Ujenzi WA Taifa la Tanzania.
Ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikutana na wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Ajenda kuu katika kikao hicho ilikuwa ni kuundwa kwa Tume ya Maridhiano ya Kitaifa itakayoratibu maandalizi ya marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa maoni yangu, hiki si kikao cha kawaida; bali ni hatua adhimu inayoweza kuamua sura na mustakabali wa siasa zetu kwa miaka mingi ijayo.
Katika kikao hicho Rais Samia alipendekeza tume hiyo iundwe kwa pamoja, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza mashauriano na wadau wa siasa, asasi za kiraia na sekta binafsi.
*Mambo kadhaa ya msingi yalijitokeza ni:*
• Kila chama cha siasa kinatarajiwa kuwasilisha majina ya watu wawili, kwa kuzingatia jinsi, kwa ajili ya uteuzi wa wajumbe wa tume.
• Viongozi wa dini watapata nafasi ya kukutana na kutoa maoni yao kuhusu mchakato wa maridhiano.
• Rais aliviomba vyama vya siasa kuwaelimisha wananchi kuhusu kazi ya tume na namna ya kuwasilisha maoni yao pale tume itakapowafikia.
• Mchakato wa maridhiano utatangulia marekebisho ya Katiba; maoni ya wananchi ndiyo yatakayobainisha maeneo yanayohitaji kubadilishwa, kisha Serikali itaandaa waraka wake.

• Wajumbe wa Baraza walipendekeza uteuzi uzingatie uwakilishi wa pande mbili za Muungano na ushiriki wa wanawake, na kwamba ripoti ya Kikosi Kazi kuhusu demokrasia ya vyama vingi isambazwe kwao.
Huu ni mwendelezo wa Vikao kadhaa tangu Uchaguzi Mkuu wa 2025 umalizike. Hii ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais kuendelea kujenga amani na umoja wa Kitaifa.
*Umuhimu wake kwa taifa: leo na kesho*
Neno maridhiano ambalo linatokana na ridhaa: Maana yake ni hali, ambapo pande zote zinaridhika.
Si ushindi wa upande mmoja dhidi ya mwingine, wala si kunyamazishana. Ni kukaa pamoja hadi kila upande uone sehemu yake katika suluhisho. Ndiyo maana nasema maridhiano ndiyo suluhu.
Kwa sasa, taifa letu linahitaji kuponya majeraha ya kipindi cha uchaguzi.
Kwa siku zijazo, Katiba inayotokana na maridhiano ina nafasi kubwa ya kudumu kuliko ile inayoandikwa na upande mmoja.
Zaidi ya hapo, mchakato huu unaweza kujenga utamaduni mpya wa kisiasa:tofauti zetu zikatatuliwa mezani kwa hoja, si mitaani wala mitandaoni kwa matusi. Huu ndio urithi aliotuachia _Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, aliyesisitiza mjadala wa wazi na umoja wa kitaifa_
*Maoni na mapendekezo ya jumla*
Meza imeandaliwa. Swali sasa ni: _tutaijaza nini na kwa namna gani?_
Mapendekezo yetu ni yafuatayo:
Mosi, sauti ya wananchi iwe kiini cha mchakato. Kama alivyodokeza Mheshimiwa Rais mwenyewe kuwa, maridhiano ya viongozi pekee hayatoshi; yanapaswa kuwa maridhiano ya taifa. Tume itakapoundwa iwafikie wananchi hadi vijijini kupitia mikutano ya wazi, redio za jamii na majukwaa ya kidijiti, kwa Kiswahili chepesi kinachoeleweka na kila mtu. Muda wa kukusanya maoni uwe wa kutosha, na muhtasari wa maoni hayo uchapishwe ili wananchi waone kuwa wamesikilizwa.
Pili, tupate wajumbe wenye sifa na upevu wa mambo. Tume hii itahitaji watu waadilifu, wenye uzoefu, wanaokubalika na pande zote, na wenye tajriba kubwa ya kusikiliza kuliko kusema.
Navinasihi vyama vya siasa vipendekeze majina kwa kuzingatia uwezo na uzalendo, si ushabiki wala kulipana fadhila.
Tatu, ujumuishi wa makundi yote. Kuzingatia jinsi katika majina ni hatua nzuri; ningependa tufikie uwiano sawa wa wanawake na wanaume. Vijana, ambao ni kundi kubwa la wananchi na wahusika wakuu wa matukio ya hivi karibuni, wanapaswa kuwa na nafasi ya dhati, si ya mapambo.
Aidha,watu wenye ulemavu, wanataaluma na wasomi, viongozi wa dini, wanahabari, wakulima, wafanyakazi, sekta binafsi, asasi za kiraia na Watanzania waishio ughaibuni. Huku uwakilishi wa Tanzania Bara na Zanzibar uzingatiwe kikamilifu.
Nne, uwazi katika kila hatua. Hadidu za rejea za tume, ratiba ya kazi zake na ripoti ya Kikosi Kazi ziwekwe hadharani. Uwazi hujenga imani; usiri huzaa minong’ono.
Tano, mlango uwe wazi kwa wote. Wadau ambao bado hawajajiunga na meza hii waendelee kukaribishwa bila masharti magumu.
Sita, lugha ya staha.Wanasiasa, wanahabari na watumiaji wa mitandao ya kijamii tuepuke lugha ya chuki, kejeli na uchochezi katika kipindi hiki. Lugha ina nguvu ya kujenga au kubomoa; tuitumie kujenga.
Saba, mapendekezo yatekelezwe. Mwisho wa safari hii uwe utekelezaji wa mapendekezo ya tume, si ripoti nyingine kabatini. Kuwe na utaratibu wa ufuatiliaji unaoweza kupimwa na wananchi.
*Hitimisho*
Dkt. Samia ameonesha njia kwa kufungua meza ya majadiliano. Jukumu sasa ni letu sote: vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia, wasomi na kila mwananchi kuijaza meza hiyo kwa hoja, hekima na uzalendo.
Kama alivyosema Rais mwenyewe, ulinzi wa amani ya Tanzania ni jukumu la Serikali, vyama vya siasa na wananchi wote. Tukifanikiwa, tutawarithisha watoto wetu si Katiba tu, bali utamaduni wa kuzungumza na kuelewana.
Mwandishi ni Mhadhiri Mwandamizi na Mshtiti wa Lugha
sovu82@gmail.com






