Na. Atley Kuni, WAF-Nkinga, TABORA
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Fistula Duniani yamefanyika leo Mei 23, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Hospitali ya Rufaa ya Nkinga huku Serikali ikisisitiza kuongeza uwekezaji katika afya ya mama na huduma za uzazi salama nchini.
Akiongea katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Waziri waAfyaMhe. Mohamed Mchengerwa, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari amesema fistula bado ni changamoto kubwa ya afya ya uzazi inayowaathiri wanawake wengi na kusababisha maumivu, unyanyapaa pamoja na kupoteza heshima katika jamii.
Amesema duniani wanawake kati ya 50,000 hadi 100,000 hupata fistula kila mwaka, huku Tanzania ikikadiriwa kuwa na wagonjwa wapya kati ya 2,500 hadi 3,000 wanaopata tatizo hilo wakati wa kujifungua.
“Wanawake takribani 1,500 hupatiwa matibabu kila mwaka nchini, hali inayodhihirisha kuwa bado kuna haja ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi hasa maeneo ya vijijini” amesema Ndugu Tayari.
Naibu Katibu Mkuu Tayari amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto kupitia upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, huduma za dharura pamoja na mafunzo kwa wataalamu wa afya.

Katika hatua nyingine, ametangaza kuiridhia Hospitali ya Rufaa ya Nkinga kuwa Hospitali ya Kanda ya Magharibi kwa huduma za fistula ili kuongeza upatikanaji wa matibabu, mafunzo na huduma za rufaa kwa wanawake wa ukanda huo.
Aidha, ameitaka Fistula Foundation kushirikiana na Serikali kujenga majengo maalumu yenye hadhi kwa ajili ya huduma za fistula ifikapo Mei 23, 2027 ili kuboresha mazingira ya tiba na urejeshaji wa utu kwa wagonjwa.
Naibu Katibu Mkuu Tayari amesisitiza umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wote akieleza kuwa mfumo huo utasaidia wajawazito kupata huduma mapema, kupunguza ucheleweshaji wa rufaa na kuongeza usawa wa huduma za afya nchini.
Tayari ametumia jukwa hilo kuwataka wananchi kutumia huduma ya “Ongea na Waziri” kutoa taarifa au kuomba msaada kuhusu changamoto za afya ya mama na fistula, huku akisisitiza kuwa ugonjwa huo unazuilika na unatibika.
Akiongea kwa niaba ya Mashirika yanayoshirikiana na Serikali, Mkurugenzi wa Fistula Foundation Clement Ndahan, ameahidi kuendelea kutoa misaada ya kifedha kati ya miaka mitano hadi kumi ijayo.
Akihitimisha hotuba yake, Ndugu Tayari ametoa wito kwa jamii kuondoa unyanyapaa dhidi ya waathirika wa fistula na kushirikiana kuhakikisha kila mwanamke anapata huduma salama za uzazi kwa wakati.






