Na. Abeid Poyo, RUJAT
Katika ulimwengu wa sasa wa habari za kidijitali na kasi ya mtandao, vichwa vya habari vingi vimekuwa vikitawaliwa na matukio ya mijini kama vile siasa za majukwaani, mabadiliko ya bei za hisa, mijadala ya kiteknolojia, na burudani.
Hata hivyo, wakati vyombo vya habari vikiangazia zaidi majiji na miji mikubwa, moyo halisi wa Tanzania unadunda kimya kimya vijijini.
Huko ndiko wanakomenyeka wakulima, wafugaji, wavuvi, na wajasiriamali wadogo wanaozalisha rasilimali zinazoliweka Taifa hili hai.
Swali la kujiuliza ni hili: Kwa nini Tanzania inahitaji habari za vijijini? Jibu ni fupi lakini zito, kwamba bila habari za vijijini, uchumi wetu unatembea kama mtu kipofu na ustawi wa taifa unakosa dira iliyosimama kwenye uhalisia.
Uchumi wa Tanzania sio wa benki za Dar es Salaam pekee; unajengwa kwenye misingi ya sekta ya kilimo, mifugo, na uvuvi ambazo hupatikana kwa wingi vijijini.
Sekta hii inaajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania. Hata hivyo, bila habari thabiti na za kina kutoka vijijini, jamii yetu inakosa taarifa muhimu za kiuchumi zinazoweza kubadilisha maisha.
Kwa mfano, hebu tufikirie mkulima wa mahindi huko Sumbawanga au mchuma korosho Masasi.
Bila vyombo vya habari kufichua changamoto za masoko, njia za usafirishaji, au bei elekezi halisi za soko la dunia, wakulima hawa huishia kunyonywa na madalali wa kati.
Habari za vijijini hutoa mwanga kwa wakulima kujua wapi pa kupeleka mazao yao, kuzuia hasara, na kuongeza tija kiuchumi.
Sambamba na hilo, wakulima na wafugaji wengi hawana ufikiaji rahisi wa huduma za kifedha, ambapo habari zinazolenga vijijini zikielimisha kuhusu upatikanaji wa mikopo nafuu ya kilimo, kama ile inayotolewa kupitia ruzuku za serikali au benki za maendeleo, huongeza mzunguko wa fedha na kukuza pato la taifa.
Utawala bora na maendeleo ya watu hupimwa kwa jinsi jamii za pembezoni zinavyoweza kupata huduma za msingi, na habari za vijijini zinasimama kama daraja kati ya wananchi na serikali.
Mara nyingi, changamoto kama ukosefu wa dawa katika zahanati za vijijini, au shule zisizo na vyumba vya kutosha vya madarasa, hazisikiki hadi pale mwandishi wa habari anapofika eneo la tukio.
Kupitia uandishi wa habari za vijijini, uongozi wa wilaya na mikoa, huhamasika kuchukua hatua za haraka, kama inavyoshuhudiwa kupitia ripoti za vyombo vya habari kuhusu mama wajawazito wanaotembea kilomita nyingi kufuata huduma ya afya.
Ripoti hizi zimekuwa chanzo cha ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo mbalimbali nchini yaliyo karibu zaidi na wananchi.
Zaidi ya hayo, habari za vijijini zenye tija sio tu zinazihusu matatizo, bali pia ni zile zinazoangazia mafanikio.

Kwa mfano, kuonyesha kikundi cha wanawake vijijini kilivyofanikiwa kujikwamua kiuchumi kupitia ufugaji wa kuku au kilimo cha mboga mboga, kunaacha funzo kwa jamii nyingine na kukuza ustawi wa ujumla.
Demokrasia ya kweli haianzi bungeni wala kwenye halmashauri za manispaa za mijini; inaanzia kwenye misingi ya vijiji vyetu ambako wananchi wanahitaji kusikilizwa.
Habari za vijijini huwapa nguvu wananchi wa kawaida kushiriki katika michakato ya uamuzi inayowahusu.
Wanapata fursa ya kueleza changamoto za ardhi, migogoro ya wakulima na wafugaji, na kuhoja matumizi ya rasilimali za halmashauri zao, jambo linalojenga utawala shirikishi unaozingatia mahitaji halisi ya wananchi wengi zaidi.
Uchambuzi huu unaamini kuwekeza na kuzipa kipaumbele habari za vijijini si hisani, bali ni mkakati thabiti wa kimaendeleo.
Tanzania haiwezi kufikia uchumi wa kati na hatimaye ule wa juu wenye tija na ustawi jumuishi, ikiwa bado kuna kundi kubwa la wananchi wake walio gizani kifikra na kukosa majukwaa ya kusikilizwa.
Vyombo vya habari, Serikali, na wadau wa maendeleo wanapaswa kuona kijiji si mahali pa kuokotea habari za matukio mabaya tu, bali ni kitovu kikuu cha uzalishaji, utajiri, na mustakabali wa Tanzania ijayo.
Abeid Poyo ni mwanachama wa Rujat anayeishi mkoani Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu: 0754990083






