Mbegu bora ni nyezo mhimu ya mafanikio kwa wakulima- RC Iringa

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewataka wananchi kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao kwa kutumia mbegu bora, kilimo cha kisasa, umwagiliaji, matumizi sahihi ya pembejeo pamoja na huduma bora za ugani kuanzia uzalishaji, uvunaji, uhifadhi hadi uchakataji wa mazao.

Mhe. Kheri ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Nanenane ngazi ya Mkoa wa Iringa yaliyofanyika katika Viwanja vya Kihesa, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ambapo amesema kuwa sekta ya kilimo ndiyo mhimili wa uchumi wa mkoa, hivyo ni muhimu wakulima wakatumia teknolojia na mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kipato.

Aidha RC Kheri amesema changamoto bado ipo kwa baadhi ya wakulima kuzalisha bila kuzingatia mahitaji ya soko, jambo linalosababisha kushuka kwa bei na kupunguza faida ya uzalishaji.

Awali Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa anayeshughulikia Uchumi na Sekta za Uzalishaji, Elias Luvanda, na Mstahiki Meya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada  wamesema jumla washiriki 87 wanashiriki maonesho hayo, zikiwemo halmashauri zote za Mkoa wa Iringa, taasisi za utafiti, kampuni za mbegu na pembejeo, taasisi za fedha, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mratibu wa Kitengo cha Uhamishaji wa Teknolojia na Ushirikiano wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Iringa, Bi. Lilian Ngusi, amewashauri wakulima kuzingatia matumizi ya mbegu bora na kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Maonesho ya Nanenane yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” yakilenga kuhamasisha wakulima, wafugaji na wadau wa sekta ya kilimo kuongeza uzalishaji wenye tija, kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya Taifa ifikapo mwaka 2050.

Also Read  Projects Launched to Reduce Conflicts Around reserved Areas

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *