Na. Mwandishi Wetu – Dodoma
Serikali imesema inaendelea kutatua uhaba wa watumishi wa kada ya afya katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, mkoani Kigoma, baada ya kupokea maombi ya ongezeko la watumishi kutoka kwa wawakilishi wa wananchi.
Akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Mjini, Profesa Joyce Lazaro Ndalichako, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuongeza watumishi wa afya kila mwaka nchini.
Kwa mujibu wa maelezo yake, kuanzia mwaka 2020/21 hadi 2025/26, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 37,921 wa kada za afya na kuwapeleka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Hata hivyo, amesema kuwa Halmashauri ya Mji wa Kasulu inaendelea kukabiliwa na upungufu mkubwa kwani ina mahitaji ya watumishi 868, huku waliopo wakiwa 343, sawa na asilimia 40, hivyo upungufu ukibaki watumishi 525 (asilimia 60).
Dkt. Dugange ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali imeajiri wataalam wa afya 5,000 na kuwagawia halmashauri zenye upungufu mkali, ambapo Kasulu Mjini imepangiwa watumishi 31.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutenga bajeti na kuajiri watumishi wapya katika kada mbalimbali za afya ili kupunguza uhaba uliopo kwenye halmashauri nyingi nchini, ikiwemo Kasulu Mjini.






