UCSAF na TARI Kuunganisha Mfumo wa TEHAMA na Kilimo

Na. Mwandishi wetu

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wameingia katika makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano yenye lengo la kuunganisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuimarisha utafiti wa kilimo, kuongeza tija na kurahisisha upatikanaji wa taarifa na teknolojia kwa wakulima nchini.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bw. Mulembwa Munaku, amesema UCSAF itashirikiana na TARI katika tafiti teknolojia za kilimo na kuwezesha matumizi ya teknolojia hizo kwa kuzingatia rasilimali zilizopo. Kwa upande wa TARI, taasisi hiyo itatoa utaalamu wa kilimo, matokeo ya tafiti, teknolojia na maudhui ya kitaalamu yatakayotumika katika mifumo ya kidijitali kwa manufaa ya wakulima.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, amesema taasisi hiyo imebuni teknolojia takribani 430 kupitia tafiti mbalimbali, lakini bado nyingi hazijawafikia watumiaji kwa kiwango kinachotarajiwa. Amesema ushirikiano na UCSAF utasaidia kusambaza teknolojia hizo kwa wakulima, kuongeza upatikanaji wa taarifa za kitaalamu na kuimarisha matumizi ya kilimo cha kisasa.

Ushirikiano huo pia unalenga kukuza matumizi ya kilimo cha usahihi (Precision Agriculture), ikiwemo matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones) na Akili Bandia (AI) katika kutambua wadudu na magonjwa ya mimea mapema, kufuatilia mahitaji ya mashamba na kutoa ushauri kwa wakulima kwa wakati.

TARI imeeleza kuwa tafiti zake zimechangia kuboresha uzalishaji wa kilimo, ikiwemo teknolojia za korosho zilizoboreshwa ambazo zimewezesha kuongeza mavuno kutoka takribani kilo 1,500 hadi kilo 6,000 kwa hekta.

Kwa zaidi ya miaka mitano (5) sasa UCSAF imetekeleza mipango mbalimbali ya kuendeleza matumizi ya TEHAMA katika sekta mbalimbali iliwemo Mawasiliano ya Simu, vyombo vya habari hususani Radio na Runinga, Elimu na huduma za jamii.

Also Read  Polisi Mkoani Iringa yawacharukia makampuni binafsi ya Ulinzi

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *