Wakulima Ulanda, Kalenga walia na kuporomoka kwa bei ya mazao

Na. Hafidhi Ally, RUJAT Iringa

Wananchi wa Kata ya Ulanda, Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, wamelalamikia kushuka kwa bei za mazao ya kilimo sambamba na kuongezeka kwa gharama za mbolea, hali wanayosema inaendelea kuwa mzigo mkubwa kwa wakulima.

Wakizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mheshimiwa Jackson Kiswaga, wananchi wa vijiji vya Mwambao, Weru, Lupalama na Kibebe walisema kuwa licha ya kutumia gharama kubwa kununua mbolea na kuzalisha mazao, bei ya mazao imeendelea kushuka na kuathiri kipato chao pamoja na ustawi wa familia zinazotegemea kilimo.

Wananchi hao pia wameiomba Serikali kuongeza upatikanaji wa mbolea za ruzuku na kuwatafutia masoko ya uhakika kwa mazao yao ili kuboresha kipato cha wakulima.

Akijibu hoja kuhusu mbolea za ruzuku na masoko ya mazao, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mheshimiwa Jackson Kiswaga, alisema Serikali inaendelea kutoa ruzuku kwa baadhi ya mbolea muhimu, ikiwemo Urea na DAP.

Alifafanua kuwa aina nyingine za mbolea ziliondolewa kwenye mpango wa ruzuku baada ya kipindi cha mpito kilicholenga kuwajengea uwezo wakulima kutumia mbolea hizo.

                        Mh. Jackson Kiswaga Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa

Aidha, Kiswaga alisema Tanzania inatumia mfumo wa soko huria, hivyo uzalishaji unapokuwa mkubwa bei za mazao hushuka kutokana na wingi wa bidhaa sokoni ambapo Serikali inaendelea na mipango ya kuweka bei elekezi za ununuzi na uuzaji wa mazao ili kulinda maslahi ya wakulima.

Katika ziara hiyo, Mbunge Kiswaga alikabidhi mabati 70 kwa Kijiji cha Mwambao kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya kijiji na nyumba ya watumishi, akiyawakabidhi kwa viongozi wa kijiji hicho.

Also Read  Mwenge wa Uhuru wahimiza Wananchi Mafinga kutunza Amani

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *