Waziri Mkuu awapongeza TARURA kwa uwajibikaji vijijini

Na. Mwandishi wetu, Tarime

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amekagua Daraja la Mto Nyathorogo lililopo katika Kijiji cha Nyathorogo, Kata ya Nyathorogo, wilayani Rorya, mkoani Mara, ambalo limejengwa kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kati ya wilaya za Rorya na Tarime.

Akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara leo Jumatano, Julai 2, 2026, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Rorya, Mhandisi Elifadhili Moses.

Mh. Mwigulu amepongeza wakala wa barabara mjini na vijijini kwa kuzingatia malengo na dira ya serikali ya uboreshaji wa miundombinu hususani barabara za vijijini kwa lengo la kuwezesha ukuaji wa sekta nyingine za kimkakati na kiuchumi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi wa ujenzi wa daraja hilo umegharimu shilingi milioni 729.2 ulianza Agosti 1, 2025 na kukamilika Februari 28, 2026.

Sehemu ya daraja lililojengwa na TARURA kuunganisha wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara

Mhandisi Moses alisema daraja hilo limejengwa kwa teknolojia ya mawe iliyowezesha kupunguza gharama za ujenzi kwa zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na usanifu wa awali, na kwamba Serikali imetenga fedha katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya ujenzi wa kingo za kulinda daraja dhidi ya athari za maji.

Naye Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege alisema daraja hilo limeondoa adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Rorya na Tarime, ambapo awali walilazimika kuvuka Mto Nyathorogo katika mazingira hatarishi yaliyosababisha ajali na kupoteza maisha.

Barabara inayoinganisha wilaya za Rorya na Tarime ambayo kwa muda mrefu ilikuwa kero kutokana na kukosa daraja

Aidha, alisema ujenzi wa daraja hilo umeboresha mawasiliano kati ya wilaya hizo mbili na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.

Also Read  Serikali yajizatiti kufikisha huduma na tiba ya saratani kufikia kanda zote

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *