Ombwe- Sauti za wananchi zinavyokosa nafasi kwenye vyombo vya habari

Na Fadhili Abdallah, RUJAT

Oktoba 31 mwaka huu Katibu Mkuu wa wizara ya Habari katibu mkuu wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo Gerson Msigwa amefungua mkutano mkuu wa Chama cha Waandishi wa habari za vijijini (RUJAT) uliofanyika mkoani Dodoma.

Akizungunza katika mkutano huo ambao pia uliambatana na ajenda ya uchaguzi ya viongozi wa RUJAT ambao watakaa madarakani kwa kipindi cha miaka minne Msigwa alisema kuwa asilimia  65 ya Wananchi wanaoishi vijijini hawafikiwi na  vyombo vya habari.

Msigwa alisema kuwa utafiti umebaini kuwa asilimia 80 ya habari zinazotangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari zinatokana na habari zinazokusanywa maeneo ya mjini na nyingi zikiwa za viongozi.

Kutokana na hilo Msigwa ambaye pia ni Msemaji wa serikali alisema kuwa RUJAT ambayo inajinasibisha na kuandika habari za vijijini kutimiza lengo lao kwani kwa sasa wananchi wanaoishi vijijini wanafikiwa na ombwe kubwa la taarifa zao kutofikiwa na vyombo vya habari.

Sambamba na hilo Msigwa aliwataka waandishi wa habari kuachana na tabia ya kurudia taarifa za kawaida au kusifu viongozi, na badala yake wafanye utafiti wa kina kuibua changamoto, fursa za kiuchumi, na mafanikio ya wananchi wanaoishi vijijini.

Pamoja na hayo Katibu Mkuu huyo wa wizata ya habari alisema kuwa Wananchi wamepoteza mvuto na vyombo vya habari na badala yake wamebaki kwenye makundi ya harakati na online media ambazo zinarushwa bila kuhakikiwa na wakati mwingine zikivunja sheria na kukiuka maadili.

Ili kukabiliana na hali hiyo alisema kuwa Utafiti unahitaji kufanyika nini kujua nini kifanyike kuwezesha waandishi wa habari kurudi kwa wananchi na vyombo vya habari vinavyotumia waandishi wa habari wenye weledi vinachukua nafasi yake kama kimbilio la jamii kujua mambo mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya nchi.

“Kwa sasa wanaharakati na wasanii ndiyo wanaosikilizwa sana na waananchi huku Waandishi wengi wakibaki kuwa wafuasi wa  wanaharakati wakiwa tayari kulinda  kulinda maslahi ya wananharakati  hata kama wananchi wanaumia ili mradi waandishi maslahi yao yatimizwe,”Alisema Msigwa.

Msemaji huyo wa serikali alisema kuwa serikali kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania (JAB) watahakikisha unandishi wa habari unabaki kwenye mipaka yake kutaaluma na weledi kwa habari zilizohakikiwa na kuwekwa mizania bila kupendelea upande wowote

Also Read  Machozi yaliyopuuzwa kitambo yapanguswa na Dkt Mwigulu

Ili kufikia huko alisema kuwa Lazima wadau wa habari wakae pamoja na kuhakikisha malengo ya vyombo vya habari yanasimamiwa na Serikali itahakikisha waandishi wa habari wanalindwa na kupewa nafasi yao ya kufanya kazi kwa uhuru (Freedom of Press).

Wakati msigwa akieleza hayo tafiti mbalimbali zinabainisha kuwa kuporomoka kwa mvuto wa uandishi wa habari kwa jamii na vyombo vingi vya habari kuandika habari mjini tafiti hizo zimebainisha kuwa kwa sasa hali ya usikivu wa vyombo vya habari vijijini ni mbaya sana.

Utafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa mwaka  2022 kupitia ripoti ya The State of Journalism Reporting in Tanzania 2022 ilichambua habari 1,863 kutoka magazeti, redio za kitaifa, redio za maeneo na televisheni na kubaini kuwa asilimia 30.1 ya vyombo hivyo vilisomwa na kutazamwa mjini   huku asilimia 22 vikisomwa na kutazamwa  vijijini.

Aidha utafiti wa Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey (TDHS-MIS) 2022, uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali umebainisha pia takwimu  ya wananchi wa vijijini wanaopata habari kupitia vyombo vya habari.

Utafiti ulipima wananchi wenye umri wa miaka 15–49 wanaotumia vyombo vya habari angalau mara moja kwa wiki ambapo matokeo yalionyesha kuwa wanawake wa vijijini asilimia 26 walisikiliza radio ukilinganisha na asilimia 42.3 wa mjini, asilimia 17.3 ya wananchi wa vijijini waliangalia televisheni ukilinganisha na asilimia 52.3 ya wananchi wa mjini walioangalia televisheni huku usomaji wa magazeti ukiwa chini ya asilimia nane kwa makundi yote.

Aidha kwa upande wa wanaume takwimu zilizonyesha kuwa asilimia 48 ya wananchi wa vijijini walisikiliza Radio ukilinganisha na asilimia 59 ya wananchi wa mjini huku asilimia 39 ya wananchi wa vijijini waliangalia televisheni ukilinganisha na asilimia 63.6 ya wananchi wa mji ambapo usomaji wa magazeti ulikuwa aslimia 16 kwa wananchi wa vijijini na asilimia 31.4 kwa wananchi wa mjini.

Also Read  Dr. Samizi akagua maandalizi ya uzinduzi wa ramani ya Afya ya mama na mtoto Africa

Nalo Baraza la Habari Tanzania (MCT) kupitia ripoti yake ya mwaka 2022 – 20233 State of the media in Tanzania ilifuatilia magazeti saba na kuja na ripoti inayoonyesha kwamba asilimia 22 ya wananchi wa vijijini ndiyo waliosoma magazeti hayo ukilinganisha na asilimia 78 ya wananchi wa mjini waliosoma magazeti yaliyohusika kwenye utafiti huo

Ripoti ya Baraza la Habari Tanzania inabainisha kuwa habari nyingi nyingi ambazo zilitangazwa kwenye magazeti hayo na hata zile zinazotangazwa na vyombo vingine  vya habari kwa kiasi kikubwa zimejiikita kutoka katika mikutano, semina na mikutano ya waandishi wa habari inayofanyika zaidi mijini.

Kisiwa cha Musila kilichoko ndani ya Ziwa Victoria katika Manspaa ya Bukoba ni miongoni mwa maeneo yenye simulizi za kuvutia zisizosimuliwa na vyombo vya habari. Picha na. Prosper Kwigize

Akizungumza katika Mkutano huo Mkuu wa RUJAT ambao ulianza kwa kongamano  la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini Mwenyekiti wa Taifa RUJAT, Neville Meena alisisitiza azma yake ya kuendeleza malengo ya RUJAT kwa kuhakikisha habari zinazohusu wananchi wa vijijini zinapewa kipaumbele.

Meena alisema kuwa katika kufikia azma ya malengo hayo taasisi hiyo imeazimia  kujenga uwezo wa kiuchumi na kiutendaji kwa wanachama ili waandike habari zenye maslahi kwa umma na kuwa na moyo wa kwenda vijijini kufanya stori badala ya kusubiri kubebwa na wadau mbalimbali.

Naye Katibu Mtendaji wa RUJAT, Prosper Kwigize alisema kuwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo kunatokana na safari zilizofanyika nchi mbalimbali ikiwemo India ambapo kipo chama kama hicho ambachi kimefanya vizuri na kuwezesha habari za vijijini vya mbali kupata nafasi kwenye vyombo vya habari.

“Tuna kazi kubwa ya kuijenga taasisi hii na waandishi wake kufikia malengo ya waaandishi kwenda vijijini lakini pia kujenga utashi na ushawishi wa vyombo vya habari kutumia habari zitakazotafutwa na waandishi hao hiyo ikiwa chachu kuambukiza uandishi wa habari za vijijini kwa vyombo vyote vya habari nchini,”Alisema Kwigize.

Ndg. Prosper Kwigize akifuatilia moja ya matukio ya onesho la ngoma za asili ya wabantu nchini Burundi zinazoshabihiana na makabila kadhaa ya mkoa wa Kigoma, Kagera, Ruvuma na Rukwa.

Baadhi ya waandishi wa habari waliipata nafasi kutoa maoni yao kuhusu ombwe la changamoto ya vyombo vya habari kushindwa kuandika habari nyingi za vijijini  walisema kuwa waandishi wengi wanapenda kwenda huko lakini mazingira ya vyombo vya habari nchini hayaruhusu matamanio hayo.

Also Read  Asilimia 65 ya watanzania wako vijijini na wanakosa habari

Ilankunda Gadi mwandishi wa habari anayefanya na kituo cha Star Tv akifanyia kazi mkoani Kigoma alisema kuwa Kufika vijiji vya mbali kunahitaji fedha za usafiri, malazi, mawasiliano na wakati mwingine vifaa maalumu hivyo Vyombo vya habari vinapokuwa na bajeti ndogo za uendeshaji, safari za waandishi kwenda vijijini zinaweza kupunguzwa na badala yake kutegemea taarifa zinazotumwa na viongozi au vyanzo vya mjini.

Sambamba na hilo alisema kuwa Vyombo vingi vya habari vina ofisi kuu, wahariri na waandishi wake katika miji mikubwa ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma,Mwanza na Arusha hali hii inafanya matukio ya mijini kuwa rahisi kufuatiliwa kuliko yale yanayotokea vijijini.

Naye Mwandishi wa habari, Robert Kakwesi anayefanya kazi mkoani Tabora alisema kuwa Sera na vipaumbele vya uhariri imekuwa sababu kubwa kwa  vyombo vya habari huweka uzito mkubwa kwenye siasa za kitaifa, shughuli za viongozi, uchumi wa mijini, michezo na matukio yenye mvuto mkubwa kwa wasomaji.

Athari za mabadiliko ya Tabia nchi maeneo ya vijijini hazipewi mkazo kama ilivyo mjini, wakati mwingine viongozi hizificha mamlaka za juu kuhusu athari hadi ziwe kubwa zaidi. Picha ni eneo la Bandari ya Ujiji Kigoma, iliyozama ziwani. Picha na. Prosper Kwigize

Kakwesi alisema kuwa Habari za vijijini kutazamwa kama zisizo na umuhimu wa kitaifa ni changamoto nyingine ya  mtazamo wa kitaaluma kwani baadhi ya wahariri wanaweza kuona tatizo la kijiji kimoja kuwa dogo  bila kuchunguza kama linaakisi tatizo kubwa linalowakabili wananchi katika maeneo mengine nchini akitolea  mfano, ukosefu wa maji katika kijiji kimoja unaweza kuwa sehemu ya tatizo pana la upatikanaji wa maji vijijini.

Katika maoni yake Mwandishi huyo wa habari alisema kuwa Maslahi ya kibiashara na matangazo kwa Vyombo vya habari imekuwa changamoto nyingine inayofanya vyombo vya habari kuelekeza nguvu kwenye maeneo yenye biashara nyingi, matangazo na wasomaji wengi., hivyo kufanya  habari zinazohusu jamii maskini za vijijini zinaweza kukosa nafasi kubwa licha ya kuwa na umuhimu wa kijamii.

Ili kukabiliana na hali hiyo mjadala mkubwa wa kitaifa utakaoshirikisha wadau mbalimbali inabidi kufanyika ili kubadili mtazamo huo na kuzipa kipaumbele pia habari za vijijini sambamba na kukabiliana na hali ya kiuchumi ya vyombo vya habari kuwezesha kutekeleza mpango huo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *