Asilimia 65 ya watanzania wako vijijini na wanakosa habari

Na. Hafidhi Ally, RUJAT Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa ametoa wito kwa waandishi wa habari na vyombo vyao kuzingatia maslahi ya jamii vijijini.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kongamano la Mawasiliano na Habari Vijijini lililoandaliwa na Chama chs Waandishi wa Habari za Vijijini (RUJAT) Msigwa amesema 65% ya watanzania wako vijijini na hawafikiwi ipasavyo na vyombo vingi vya habari nchini.

Amebainisha kuwa kwa sasa takribani 85% ya vyombo vya Habari viko mjini na vinatoa kipaumbele kwa habari za mjini

Akielezea umhimu wa habari za vijijini amepongeza kuanzisha Chama cha cha waandishi wa habari na kukitaka kufanya utafiti wa namna habari za vijijini zinavyopewa kipaumbele na kuanzisha mkakati wa namna ya kufanya maboresho zaidi

Msigwa amesema waandishi wanapaswa kurejea misingi ya uandishi wa habari unaolenga jamii, akitolea mfano uzoefu wake wa awali katika kuandika habari zilizobeba changamoto na mahitaji ya wananchi.

Ameeleza kuwa RUJAT ni taasisi ambayo imekuwa ikihitajika kwa muda mrefu, akisema uwepo wake utasaidia kuibua changamoto zinazowakabili wananchi waishio vijijini ambao ni zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, kwa mujibu wa maelezo yake.

Baadhi ya wanachama wa RUJAT wanaohudhuria Kongamano la mwaka la Waandishi wa habari za Vijijini 2026

Naye Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena, amewataka wanahabari walioshiriki kongamano hilo kuwa mfano katika kuimarisha uandishi wa habari wenye tija kwa kuanzia na changamoto zinazowakabili wananchi katika jamii zinazowazunguka.

Meena amesema mwandishi wa habari anapaswa kuwa sauti ya wananchi badala ya kuwa sauti ya viongozi, akieleza kuwa falsafa hiyo ndiyo msingi wa kuanzishwa kwa chama hicho.

Also Read  Wananchi Mafinga wapinga mwekezaji kupewa Hekta 400 bila ridhaa yao

Akitoa taarifa ya chama, Katibu wa RUJAT, Prosper Kwigize, amesema chama hicho kilianzishwa na wanahabari 20 kabla ya kusajiliwa rasmi, huku hadi sasa kikiwa na wanachama zaidi ya 120.

Ameongeza kuwa chama hicho kimepokea maombi mapya zaidi ya 60 ya wanachama, hatua inayolenga kuongeza nguvu katika kuimarisha nafasi ya taarifa zinazohusu maisha ya wananchi wa vijijini katika vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali ya mawasiliano.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *